Wakulima, wafugaji wapewa angalizo

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:35 AM Nov 29 2024
NAIBU Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Hamza Khamis
Picha: Mtandao
NAIBU Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Hamza Khamis

NAIBU Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Hamza Khamis amewataka wakulima na wafugaji nchini kufanya shughuli zao bila kuharibu mazingira.

Alitoa rai hiyo jana jijini Dodoma wakati akiongoza kikao na Ujumbe wa Tanzania ambao utashiriki katika Mkutano wa 16 wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame unaotarajiwa kufanyika jijini Riyadh, Saudi Arabia.

Khamis alisema vitendo vya baadhi ya wakulima kukata miti ovyo na kuchoma misitu kwa ajili ya kuandaa na kusafisha mashamba na wafugaji kulisha mifugo kiholela, huchangia ukame na hatimaye kuwapo tishio la maeneo mengi kuwa jangwa.

Naibu Waziri aliwataka wakulima na wafugaji nchini kuacha kuhamahama kwa kuwa kitendo hicho kinachochea hatari ya kuenea kwa jangwa.

"Wakulima na wafugaji wanapokata miti na kulisha mifugo, wanapohamahama wanaacha maeneo yakiwa yameharibiwa, hivyo ninawaomba waache kufanya hivyo, wanasababisha maeneo mengi kukabiliwa na hali ya ukame na jangwa," alisisitiza.

Khamis alisema pamoja na kuwa ufugaji na kilimo ni sekta kubwa zinazokuza uchumi na kutangaza nchi, wafugaji na wakulima wanao wajibu wa kuhakikisha wanafuata sheria za mazingira na hivyo kupunguza ongezeko la jangwa.

Aliwaomba wafugaji waache kuchunga au kunywesha mifugo kwenye vyanzo vya maji kwa kuwa kwa kufanya hivyo, wanasababisha uharibifu wa mazingira, maji kukauka na kuleta ukame.

Naibu Waziri huyo pia aliwasisitiza wafugaji na wananchi kwa ujumla kupanda miti na kuitunza ili kusaidia kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi yanayoikumba nchi na dunia.

Alisema hali ni mbaya kwa sababu maeneo mengi wananchi wamekata miti ovyo na kuchangia ukosefu wa mvua na hivyo ukame kukithiri katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Hivyo, Naibu Waziri Khamis alisema kuwa kukabiliana na changamoto ya uharibifu wa mazingira, serikali itaendelea na jitihada za kuwa na mpango wa matumizi ya ardhi pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kuacha shughuli zinazosababisha uharibifu wa mazingira.

Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais, Abdallah Hassan Mitawi, alisema mkutano huo wa kupambana na hali ya jangwa ni muhimu kwa Tanzania.

Alisema Tanzania kupitia wataalamu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, wizara za kisekta na wadau wa maendeleo itakuwa katika nafasi nzuri ya kushiriki kikamilifu kwa mustakabali wa nchi.  

Kikao hicho kilihudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Agnes Meena na wataalamu mbalimbali kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, wizara za kisekta na Mkurugenzi wa Taasisi ya LEAD Foundation, Njamasi Chiwanga.