Kocha wa Simba atua Asante Kotoko ya Ghana

Logarusic, kwa siku za karibuni alikuwa akiwaniwa na mabingwa wa Afrika Mashariki na Kati, Azam FC ambao wamemtimua kocha wao Zeben Hernandez.

Taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa klabu hiyo ya Ghana, imeeleza kuwa sehemu ya makubaliano hayo ni kuwa Logarusic atapewa 'fungu la fedha' pamoja na kuongezewa mkataba kama ataiwezesha timu hiyo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Ghana.

Katika taarifa hiyo, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Kwame Kyei, alisema wamemchukua Logarusic wakiamini ana uwezo mkubwa wa kuisaidia timu hiyo.

"Tunataraji atainua uwezo wa wachezaji na kujenga umoja, tunaomba tumpe sapoti pindi atakapoanza kazi muda wowote kuanzia sasa baada ya kukamilisha taratibu za vibali," alisema Kyei.

Baada ya kuondoka Simba mwaka 2014, Logarusic alienda Kenya na kufundisha timu za AFC Leopards na Gor Mahia kabla ya kwenda kujiunga na wababe hao wa Ghana.

Kotoko ina rekodi ya kutwaa ubingwa wa Ghana mara 24 huku ikitwaa Kombe la Ligi ya Mabingwa Afrika mara mbili