Watoto wenye ugonjwa wa moyo wanyanyapaliwa

18Nov 2017
Rahma Suleiman
Nipashe
Watoto wenye ugonjwa wa moyo wanyanyapaliwa

DAKTARI bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto katika Hospitali ya Mnazimmoja mjini Zanzibar, ameonya juu ya tabia ya kuwanyanyasa watoto wenye maradhi ya moyo.

Akizungumza na Nipashe , Dk. Omar Mohammed, alisema , wagonjwa wa moyo wanalalamika kuwa hivi sasa kumezuka mazoea ya unyanyapaa kwa familia zenye watoto wanaougua magonjwa wa moyo.

“Familia zenye watoto waougua ugonjwa wa moyo wamekuwa wakinyanyapaliwa na baadhi ya wanajamii na kuonekana kuwa kuuguwa maradhi hayo ni laana wakati ugonjwa huo unaweza kumpata yeyote.”

“Napenda kuiasa jamii kuachana na fikra potofu kwa familia zenye watoto wenye maradhi ya moyo kwani unapomnyanyapaa mgonjwa ndivyo unavyomsababishia , ugonjwa kwa kuwa unamwathiri kisaikolojia,”alionya.

Aidha, kuna haja ya Zanzibar kufanywa utafiti ili kujua sababu ya watoto wengi kuuguwa ugonjwa wa moyo na kwamba asilimia 45 ya watoto huathirika wakiwa tumboni na wanapozaliwa tayari wanakuwa wagonjwa wa moyo kutokana na sababu mbalimbali.

Kadhalika, ugonjwa wa moyo unasababishwa na mambo mbalimbali ikiwamo umaskini unaosababisha hali duni za maisha kwa Wazanzibari wengi.

“Umaskini unaweza kuchangia kwa sababu mama anapokuwa mjamzito mtoto anahitaji kila kitu sasa kuna vitu vikakosekana katika mlo wa kila siku vinaweza kuchangia”alisema.

Aidha, msongo wa mawazo kwa mama mjamzito unaweza kumpata mtoto, pia matumizi holela ya dawa wakati wa ujauzito ikiwemo dawa za miti shamba na za hospitali yanachangia ugonjwa wa moyo kwa watoto.

Bingwa alieleza kuwa maradhi ya kuambukiza pia yamekuwa yakisababisha ugonjwa wa moyo kwa watoto kwani mama mjamzito akiwa na maradhi ya kuambukiza mtoto anaweza kuathirika pia.

Alisema Zanzibar inaidadi kubwa ya watoto wanaoguwa ugonjwa wa moyo na iwapo utafanywa utafiti huenda idadi itakuwa kubwa zaidi.

Mohammed alisema ugonjwa wa moyo unapunguza kasi ya nguvu kazi ya taifa kupunguwa kwa sababu mtu anayefanyiwa upasuaji wa moyo hana uwezo wa kufanya baadhi ya kazi ikiwamo ulinzi hivyo hawezi kuwa askari, polisi au injinia.

Alisema kutoka mwaka 2015 hadi 2017 kulikuwa na watoto 69 waliopelekwa Israeli kutubiwa na wagonjwa 29 walipelekwa India.

“Tudumishe usafi kwa sababu usafi unapunguza maradhi ya ngozi na kwa maana hiyo unapunguza mtoto kutopata maradhi ya moyo,ninawashauri wazazi kuwadhibiti watoto kutumia vitu baridi kama barafu na maji baridi kwani unapokula vitu baridi unapunguza kinga za mwili kooni”alishauri.

Alitaka jamii kuwa na utamaduni wa kutumia vyakula na vinjwaji halisi na kuacha vyakula vya viwandani hasa kwa watoto kwa sababu mtoto unapompatia tunda halisi unamsaidia kupata vitamini na kujenga afya zao.