Walia na polisi kifo cha ndugu yao

Wakizungumza na Nipashe nyumbani kwa marehemu juzi, wanafamilia hao walisema tukio hilo limewaachia simanzi kubwa kutokana jinsi ndugu yao alivyouawa.

Kaka wa marehemu, Mohamed Mkangara, alisema siku ya tukio hilo wakati mdogo wake akitokea katika kijiji cha Mkuzi kwenda nyumbani kwake, alipofika katika shamba lake alikutana na kundi la watu likiwa na mapanga na mbwa na kuanza kumfukuza kama mhalifu.

Mkangara alisema ndugu yake alipoona kundi hilo la watu linamfukuza na mbwa, alikimbia huku akipiga kelele za kuomba msaada lakini hakufanikiwa kupata msaada wowote.

Alisema baadaye aliishiwa nguvu ndipo kundi hilo lilipomkamata na kuanza kumcharanga mapanga katika sehemu mbalimbali za mwili kisha kumwacha akiwa anatokwa na damu kwa wingi.

Aliongeza kuwa baada ya kundi hilo kumwacha akiwa hoi, wasamaria wema waliomwona akifanyiwa unyama huo walitoa taarifa polisi hatimaye kufika na kumpeleka katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Muheza, lakini alifia njiani kutokana na kutokwa damu nyingi.

Naye baba mdogo wa marehemu, Mganga Mkangara, alisema licha ya mwanawe kufanyiwa unyama huo, hakuwa na ugomvi na mtu yeyote zaidi ya kwamba alikuwa akilalamika kuibiwa na kuharibiwa mazao yake shambani na watu wasiojulikana.

“Tunaliomba jeshi la polisi lifanye uchunguzi wa kina ili kuwabaini watu waliohusika na mauaji hayo ya kinyama ili sheria ichukue mkondo wake dhidi ya wahusika wote," alisema Mkangara.

Alisema licha ya kwamba ndugu yao ameshakufa, wanaomba haki itendeke kwa hatua kali kuchukuliwa kwa wahusika wote.