Dk. Tulia afundisha wasichana mbinu kuwakwepa ‘mafataki’

16Jul 2017
Nebart Msokwa
Nipashe Jumapili
Dk. Tulia afundisha wasichana mbinu kuwakwepa ‘mafataki’

NAIBU Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Tulia Akson na Mbunge wa Viti Maalumu kupitia Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM)-

Mkoa wa Dodoma, Mariam Mzuzuri, wamewapa wanafunzi wasichana mkoani Mbeya mbinu kadhaa za kukwepa ‘mafataki’ wanaowarubuni ili kujiweka mbali na hatari ya kuharibiwa maisha yao.

Tulia na Mazrui walitoa somo hilo mwishoni mwa wiki kwa nyakati tofauti walipofanya ziara kwenye shule mbalimbali mkoani Mbeya na kufanya mazungumzo na wasichana, lengo likiwa ni kuwataka waepukane na mimba wakiwa shuleni na kuharibu maisha yao.

Walieleza kuwa Serikali imeshatoa msimamo wake wa kutoruhusu waliojifungua kurejea kwenye shule zake na hivyo, wanapaswa kujitunza na kujiweka mbali na masuala ya mapenzi bali kuongeza juhudi katikia masomo yao.

Dk. Tulia na Mzuzuri walifanya ziara hiyo katika shule za Sekondari Loleza ambayo ni ya wasichana na pia ya Wazazi Ivymwe, zote za jijini Mbeya. Walitembelea pia katika Shule ya Wasichana ya Kayuki iliyopo wilayani Rungwe ambako waliongozana na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako.

Dk. Tulia aliwataka wasichana hao kuepuka kushika mambo mawili kwa wakati mmoja, kwa maana ya elimu na mapenzi kwa sababu upo uwezekano mkubwa wa kushindwa katika yote, na hasa elimu.

Aliwakumbusha kuwa hata wao waliwahi kuwa wasichana kama walivyo wanafunzi wa sasa, na walikuwa wakitembea umbali mrefu kwenda shuleni kutokana na shule kuwa chache tofauti na ilivyo sasa, lakini bado walifanya vizuri baada ya kushinda dhidi ya vishawishi na vikwazo vingi walivyokuwa wakikumbana navyo.

Aliwataka kuacha kumiliki simu wawapo shuleni kwa vile nyingi ndizo huwa chanzo cha wengi wao kupata mimba kutokana na kuwa na mawasiliano na watu wanaorubuni wasichana na kuwaharibia maisha.

“Katika Shule ya Loleza kuna baadhi ya wasichana ambao walifukuzwa kwa sababu ya mimba. Lakini walipochunguzwa ilibainika kuwa ni walewale waliokuwa wanakimbizana na walimu kutokana na tabia zao za kumiliki simu,” alisema Dk. Tulia.

Kwa upande wake, Mzuzuri aliwataka wasichana kuzingatia kanuni ya magauni manne katika maisha yao ambayo ni sare ya shule, joho la kuhitimu Chuo Kikuu, shela la harusi na dera.

Alisema magauni hayo yanafuatana kwa mtiririko huo huo na kwamba endapo mwanafunzi ataharibu mtiririko huo kwa kuruka hatua, atakuwa amejiharibia maisha yake.

“Mwanafunzi anayenyonyesha ni vigumu sana kuzingatia masomo kwa sababu kuna maudhi mengi katika uleaji wa mtoto mchanga. Kwa vyovyote vile, ataacha kusoma. Atakuwa anawaza mtoto wake amekula nini, mtoto anaumwa na kwenda kumnyonyesha,” alisema Mzuzuri.

Habari Kubwa