Wazuiwa kutumia mizani isiyo na vigezo

Maofisa vipimo kutoka Wakala wa Vipimo (WMA), wamesema ukaguzi mwingine utafanyika ili kubaini kama imefikia viwango vya matumizi na kubandikwa alama maalumu.

Katika ukaguzi uliofanyika Wilaya ya Ruangwa, WMA ilihakiki Vyama vya Ushirika vya msingi (AMCOS) 23 na kukagua mizani 150 na kati ya hiyo iliyopimwa na kuhakikiwa ni 56 na iliyozuiliwa kutumika mpaka itakapofanyiwa marekebisho ni 94.

“Mizani mingi imeonekana kuwa na upungufu (haipimi sahihi) kwakuwa ilibainika baadhi ina upungufu kuanzia gramu 200 hadi kilo moja ambayo kwa kawaida mzani unatakiwa kuwa na upungufu unaokubalika wa gramu 80 tu,” ilifafanua WMA.

Aidha, baadhi ya mizani imechakaa na kusababisha kupoteza usahihi katika upimaji kutokana na jinsi mizani hiyo inavyohifadhiwa katika maeneo machafu yenye vumbi ambayo husababisha kupata kutu.

Kadhalika njia inayotumika kusafirishia mizani hiyo si salama kwa kuwa usafiri unaotumika mara nyingi ni pikipiki zinazosababisha kuangusha baadhi ya vifaa muhimu.

Meneja wa mkoa WMA, Stephen Masawe, alisema wameamua kuendeshea ukaguzi huo ili kurekebisha kasoro mbalimbali zilizokuwa zikisababisha mkulima kupunjwa.

Baadhi ya wananchi wameipongeza WMA kwa kuwapa elimu ya matumizi sahihi ya vipimo na kufanya ukaguzi.