|
Jamhuri kusimamia usajili Simba 2008/09
2008-05-11 10:57:30
By Mwandishi Wetu
Kocha msaidizi wa timu ya Simba Jamhuri Kihwelu amekabidhiwa jukumu la usajili wa wachezaji kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kuu ya Bara, imeelezwa jijini mwishoni mwa wiki.
Mweka Hazina msaidizi wa klabu ya Simba Chano Almas alisema jijini baada ya kwenda mapumziko kwa kocha mkuu Milovan Cirkovic, sasa watamtumia Jamhuri kukamilisha zoezi hilo.
Almas alisema Milovan alitoa mapendekezo ya kuachwa kwa wachezaji kadhaa, hasa wale walio majeruhi wa mara kwa mara na nafasi zao zichukuliwe na wengine aliowaona katika timu nyingine za ligi kuu.
Hata hivyo Almasi alikataa kuwataja wachezaji hao.
``Kocha kaacha maelekezo ya usajili na hatuna shida kwa kuwa alikuwa pamoja na Jamhuri katika kazi ya kufundisha, basi ndiye atakayechukua jukumu hilo mpaka kocha akirudi kwenye Juni,`` alisema Almasi na kueleza zaidi, ``tutaendelea na zoezi hilo kwa ufanisi.``
Almasi, hatahivyo, hakuweza kuthibitisha kama Cirkovic atarudi kwa kusema ``Hatujui. Yeye ni binadamu. Lolote linaweza kutokea.``
Kumekuwepo madai kuwa `Mzungu` huyo hatorudi kwasababu Simba itakuwa na mechi za nyumbani tu msimu ujao baada ya kushika nafasi ya tatu kwenye ligi kuu ya Bara.
Aliwataja wachezaji waliokuwa majeruhi wa vipindi virefu wakati wa ligi kuwa ni Nurdin Bakari, Nassor Salum `Cholo` na Victor Costa, ``lakini wameshapona isipokuwa Costa anaendelea na matibabu.``
Nurdin, hatahivyo, ni mmoja wa wachezaji wawili waliokaririwa wiki iliyopita wakisema hawako tayari kuichezea tena Simba msimu ujao baada ya kusimamishwa kwa utovu wa nidhamu wa kudai mishahara ya miezi miwili muda mfupi kabla ya kumalizika kwa ligi kuu ya Bara mwezi uliopita.
|