11 May 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Sportsnews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Ngassa ajiapiza kutoihama Yanga
 
2008-05-11 10:56:56
By Mwandishi Wetu

Winga machachari wa Yanga na timu ya taifa, Taifa Stars, Mrisho Ngassa amesema kamwe hatoihama klabu hiyo msimu ujao na kujiunga na timu nyingine yoyote ya ligi kuu ya Bara licha ya kufuatiliwa kwa karibu na Mtibwa Sugar na Kagera Sugar.

Timu za Mtibwa Sugar na Kagera Sugar ambazo zinamilikiwa na kampuni moja zimeingia katika vita kali ya kumuwania mshambuliaji huyo.

Ngassa aliliambia Lete RAHA kuwa ana wakati mgumu kutokana na timu hizo mbili kupigana vikumbo kumtaka amwage wino kwa ajili ya kuzichezea kwenye ligi kuu msimu ujao.

``Hili limekuwa tatizo sasa kwani hizi timu ni ndugu, na pia Kagera nilishawahi kuichezea. Lakini kwa sasa bado sina mawazo ya kuondoka Yanga na kwenda tena katika timu nyingine ya hapa nyumbani,`` alisema Ngassa ambaye aliitwa kwenye timu ya taifa baada ya mashabiki kupiga kelele kwa muda mrefu.

Ngassa ambaye ametoa mchango muhimu kwenye timu hiyo tangu achukuliwe mapema mwaka huu, ikiwemo kiwango kilichosaidia kuifunga Uganda 2-0 mjini Mwanza mwishoni mwa wiki iliyopita alisema, hatahivyo, ``napenda zaidi nikacheze soka la kulipwa nje ya nchi (baada ya Yanga).``

Aidha, uongozi wa Yanga pia umeahidi kuwa hautakuwa tayari kumuachia kwa gharama yoyote.
Katika mchezo huo wa Stars Ngassa alitoa pasi za uhakika ikiwemo iliyozaa bao la kwanza la timu hiyo lililofungwa na Emmanuel Gabriel.

Ngassa mshambuliaji mwenye chenga za maudhi, kabla ya kujiunga na Yanga alitokea Kagera Sugar ambayo aliichezea msimu mmoja tu baada ya kung`ara akiwa na Toto African ya Mwanza iliyokuwa ikishiriki ligi daraja la kwanza.

Alipoulizwa juu ya mipango ya kumchukua Ngassa tena, kocha mkuu wa Kagera Sugar Syvestre Marsh alisema hana taarifa.

``Sijui kama uongozi unamtaka arudi Kagera. Lakini nimekuwa nikifurahishwa na maendeleo mazuri ya Ngassa ndio maana nilitoka naye Serengeti Boys, Ngorongoro Heroes na baadaye Kagera Sugar,`` alisema Marsh.

Hakuna kiongozi wa Mtibwa Sugar aliyepatikana kuzungumzia jitihada za timu hiyo kumsajili winga huyo.

  • SOURCE: Lete Raha
TODAY
-----------------------------------------------
Editorial
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.