|
Kondic:Hakuna wa kucheza Yanga Taifa Cup
2008-05-11 10:55:46
By Mwandishi Wetu
Kocha mkuu wa mabingwa wa soka wa Bara Yanga Dusan Kondic amesema hajaona mchezaji mwenye kiwango cha kuichezea timu yake kwenye mashindano yanayoendelea jijini Dar es Salaam ya Kombe la Taifa.
Kondic ambaye amekuwa akihudhuria michuano hiyo kwenye Uwanja wa Taifa tangu kuanza kwake mapema wiki hii, aliiambia Lete RAHA katika mahojiano maalumu kuwa ameona si chini ya mechi tano lakini hakuna mchezaji aliyemvutia.
Hakuna mchezaji mwenye kiwango kizuri cha kutosha kusajiliwa kwenye kikosi cha timu yake kwa ajili ya msimu ujao, alisema Kondic.
``Nimekuwa nikija tangu kuanza kwa mashindano haya, lakini bado sijapata mchezaji wa aina ninayotaka,`` alisema Kondic uwanjani hapo mwishoni mwa wiki.
``Wengi wao bado viwango vyao vipo chini na stamina pia hamna.``
Mikoa mingi imeonyesha kiwango cha chini mno cha mchezo kilichofikia ukomo katika ushindi wa mabao 10-1 wa Ilala dhidi ya Lindi.
Ukiacha timu zilizosheheni wachezaji wa klabu za ligi kuu ya Bara kama Ilala, mikoa mingi, ikiwemo Lindi, imejaa wachezaji ambao wameathiriwa na uamuzi usio wa busara wa shirikisho la soka, TFF, wa kuvunja ligi za madaraja ya chini.
Kutokana na kutokuwepo kwa ligi za madaraja ya chini, timu za Iringa, Manyara, Kigoma, Ruvuma, Tabora na Lindi zilionyesha kiwango cha chini cha soka kilichoambatana na ukosefu wa stamina na kuwa-fiti-kimechi.
Hatahivyo, Kondic alisema ataendelea kuudhuria kwenye mashindano hayo yanayotarajiwa kumalizika Mei 24 kuona kama kutakuwa na mabadiliko ya kiwango. Mechi za hatua ya mtoano zinaweza kupandisha uchezaji wa baadhi ya wachezaji.
``Nadhani baadaye ninaweza kupata mchezaji au wachezaji wa nafasi ninazozitaka kwani hatua zinazokuja ni nzuri zaidi,`` alisema Kondic ambaye, kwamfano, aliondoka wakati wa mapumziko wa mchezo kati ya Ilala na Lindi mabao yakiwa 7-0.
Ilala inajumuisha wachezaji wengi wa timu mbili kubwa nchini za Yanga na Simba.
``Hakuna jipya. Simba nimewaona mara nyingi kwenye ligi, sioni jipya hapo,`` alisema.
Yanga inafanya usajili ikiwa na lengo la kufanya vizuri kwenye Kombe la Kagame la Juni, Kombe la Tusker la Agosti na msimu mpya wa ligi kuu ya Bara utakaoanza Septemba. Itacheza pia Ligi ya Klabu Bingwa Afrika kuanzia Februari, mwakani.
|