|
Chaka apinga kushindwa Manyara
2008-05-11 10:54:19
By Bahati Mollel
Kinara wa mapinduzi yaliyoshindwa ya uongozi kwenye chama cha soka cha mkoa wa Manyara, MARFA, Omar Chaka amekata rufaa kwenye kamati ya michezo ya mkoa huo akipinga kushindwa pia katika uchaguzi wa chama hicho uliofanyika hivi karibuni kwa kuwa haukufuata katiba.
Chaka ambaye pia ni mwenyekiti wa chama cha wilaya ya Babati, BDFA, alisema jijini juzi Ijumaa alipinga uhalali wa kufanyika kwa uchaguzi huo baada ya kuona katiba imevunjwa na taratibu nyingine zilikiukwa na kamati ya michezo ya mkoa katika uchaguzi huo.
Hatahivyo, alisema, kamati iliwataka kuwasilisha malalamiko rasmi baada ya uchaguzi huo.
Alisema katiba ya MARFA inawataka wapiga kura kuwa wawili kutoka kila chama shirikishi na klabu, lakini katika uchaguzi huo walitoa wajumbe watatu-watatu.
Aidha Chaka alisema kamati ilikubali wapiga kura ambao klabu zao hazijasajiliwa na msajili wa vyama na klabu za michezo nchini.
``Katiba tunayoendelea kutumia ni ile ya mwaka 2004, sasa ni maajabu kwani hao wasimamizi wanaonekana kuwa na lao jambo kwani walitaka mambo yaende haraka haraka, na walifanikiwa na uchaguzi ukafanyika,`` alisema Chaka.
Chaka alianguka katika nafasi ya katibu mkuu baada ya kupata kura tatu kati ya 11 zilizopigwa.
Alisema pia kamati hiyo ilikataa kufanyika kwa mkutano mkuu wa uchaguzi ambao ungetakiwa kutoa taarifa mbalimbali ikiwemo ya fedha kwa kipindi cha miaka mitatu ya uongozi uliopita.
Pia alisema pia kamati hiyo ilichukua jukumu la kutoa na kupokea fomu za uchaguzi yenyewe, wakati zoezi la utoaji lilitakiwa lifanywe na MARFA.
Chaka alisema pia Mwenyekiti aliyechaguliwa Charles Mugodo alitakiwa jina lake liondolewe wakati wa usaili kutokana na kuvunja katiba kwa kupeleka masuala ya michezo mahakamani ingawa baadaye alifuta kesi hiyo aliyokuwa akimdai Chaka fidia ya shilingi milioni 100 kwa kumkashfu.
Wanamichezo wengine walioorodheshwa kupinga uchaguzi huo pamoja na Chaka ni mjumbe wa mkutano kuu wa BDFA, Peter Yaghambe, Makamu mwenyekiti, Katibu na mjumbe Mbulu, Christopher Kalimba, Fortunatus Kalewa na Silven Bura, Mwenyekiti na mjumbe Kiteto J. Kidukuli na Mohamed Bin.
|