|
Wasanii watoe `contact` kwa mashabiki
2008-05-11 10:53:13
By Amour Hassan
Cheo ni dhamana, Waswahili waliwahi kusema enzi hizo kabla msamiati wa sasa wa kisiasa wa `FISAD` haujaingia; Mzee wa Busara anakumbuka. Lakini katika ulimwengu wa Bongofleva, wa muziki wa kizazi kipya, umaarufu wa msanii ndiyo dhamana.
Msanii, hasa akiwa maarufu, apende asipende, atakuwa na mashabiki ambao kwa kufarijika kwao na tungo zake, humuona kuwa ni rafiki wa karibu mno.
Kwa waliopagawa zaidi na kazi za msanii husika, mwenyewe apende asipende, humchukulia msanii huyo wampendae kwa ukaribu zaidi. Kama ndugu f\'lani hivi.
Kwa wenye nia ya kum-\'fisad\' msanii husika waliyevutiwa na kazi zake na mwili wake, na ambaye mara nyingi huwa ni wa jinsia tofauti na ya fidadi mwenyewe, humtamani msanii husika.
Makusudio ya aina zote tatu, hatahivyo, yanaunganishwa na ukweli mmoja ambao hauepukiki. Nia ya mashbiki ya kujenga mawasiliano, ikiwezekana ya kudumu.
Lakini, tofauti na wasanii wasio wa Bongofleva ambao ni rahisi kupatikana katika kumbi ambazo bendi hutumbuiza mpaka mara tano kwa wiki, wasanii wengi wa muziki wa kizazi kipya huwa ni vigumu kupatikana.
Wanapopatikana, baadhi, huwa wagumu pia kuweka wazi njia ya mawasiliano ya kupatikana kwao.
Matokeo yake?
Matokeo yake, karibu kila wiki, Mzee wa Busara amekuwa akipokea maombi zaidi ya matano ya mashabiki wenye nia ya kuwasiliana na wasanii wawapendao, kwasababu yoyote.
Hii ni ishara ya tatizo.
Kutofahamika kwa mawasiliano ya wasanii wengi wa Bongofleva, wakiwemo magwiji wenye majina makubwa kuliko hata fani yenyewe pengine, ni tatizo kwasababu, kwanza, haikutakiwa kuwa hivyo.
Kama ambavyo Mzee wa Busara alitangulia kusema awali, umaarufu wa msanii wa kizazi kipya ni dhamana. Na kwa jinsi hiyo, ni wajibu wa msanii wa Bongofleva kuwa tayari kutibu kiu ya mashabiki wake wakati wowote na mahali popote na wenzetu, hasa wa majuu, wanafanya.
Kila jambo lina faida na hasara, na kama ambavyo nia za mashabiki katika kutafuta mawasiliano na wasanii wa Bongofleva zimetofautiana mara tatu, kumeambatana na raha na karaha.
Lakini kwasabsbu umaarufu ni dhamana, na kwasababu hakuna maisha ya msanii kisanii bila upendo wa mashabiki wake, kufahamika kwa njia ya mawasiliano ni jambo la lazima. Piga ua.
Piga ua, msanii wa Bongofleva ana jukumu la kushirikiana na wapenzi wake kwa ajili ya kuendelea kuwashika wale ambao ameshawashika katika hali ya kirafiki, na undugu kwa waliopagawa zaidi. Ndiyo ubinadamu ulivyo.
Piga ua, msanii anahitaji kupanua wigo wake wa mawazo, ideas, za kufanyia kazi kwa nia ya kutoa kazi zilizo bora zaidi ama za ubora uleule mara kwa mara.
Na hili litabanwa, kwa vyovyote, kama wigo wa mawasiliano wa msanii na jamii unaishia katika washikaji wa kijiweni na wa kwenye studio za kurekodia.
Piga ua, msanii anahitaji kupanua wigo wake wa mawasiliano ili kujijenga ama kuendelea kujenga uwezo wake kibiashara, na hapa ningependa kutoa mfano wa msanii mmoja wa kike ambaye, katika mahojiano na kituo kimoja cha redio, aliwahi kusema alipata kazi za nje ya nchi za kila mwaka baada ya promota kuwasiliana na meneja wake kwa njia ya mtandao wa kompyuta.
Huenda Mzee wa Busara hana hakika na idadi kamili ya wasanii wa Bongofleva wenye mitandao ya kompyuta au wenye kutumia mitandao ya kompyuta kimawasiliano.
Lakini ambacho Mzee wa Busara ana uhakika nacho ni kwamba ni idadi ndogo sana ya mashabiki na mapromota ambao wanafahamu mawasiliano hayo.
Kufungua mtandao wa kompyuta kuna gharama zake na si busara Mzee wa Busara kushauri kila msanii wa Bongofleva afungue mtandao wa mawasiliano ya kompyuta.
Ambacho Mzee wa Busara anaona ni busara kushauri kwa manufaa ya wasanii wenyewe na kiu ya mashabiki wengi wa muziki wa kizazi kipya, ni kwa wakali husika kufanya kila jitihada katika kutambulisha e-mail adress zao kwa jamii.
Matumizi ya e-mail adress yana udhaifu wake hasa kwa nchi ya dunia ya tatu kama Bongo, Mzee wa Busara anafahamu. Ni teknolojia inayohusisha wapenzi wachache, kwa uchache.
Lakini wasanii wa Bongoflava hawapaswi kuachwa na muda kutokana na faida nyingi zilizo katika mawasiliano ya njia hiyo.
Kwa kuwasiliana kwa e-mail iliyotangazwa vizuri kutamsaidia msanii kutuliza kiu ya mashabiki wake ambayo ni lazima itulizwe kwa manufaa ya msanii mwenyewe.
Lakini la ziada ni kuwa njia hiyo itawasaidia kuchuja mawasiliano yenye nia ya kuzalisha bugudha zinazotokana na matamanio ya kimahusiano. Iwe kwa ma-men au mademu.
|