11 May 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Sportsnews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Spidi 120 anayesambaza bata kila sehemu na nge 1982
 
2008-05-11 10:52:36
By Amour Hassan

Mkali amerejea kwa spidi ile ile 120. Ndivyo ambavyo unaweza kumuelezea Ngwair kwa haraka haraka juu ya kazi zake mpya baada ya kutangaza kujitoa katika gemu mwaka 2006.

Tangu arejee, Ngwair ameendelea kuonyesha kuwa vitu vikubwa alivyovifanya katika albam yake ya kwanza - wakati akiibuka katika gemu ya Bongofleva - havikuwa vya kubahatisha.

Alibamba ki-aina kwa songi lake la kwanza la marejeo katika gemu la `Singida Dodoma`, akatingisha tena kwa pini la kiwango cha kuvuka mipaka la `She Performs` aliloliimba katika lugha ya Kiingereza akimshirikisha TID na sasa yuko hewani tena akiing`arisha remix ya traki `Hapo Vipi` ya Profesa Jay iliyowashirikisha wakali wengine kama Mwana FA, Chid Benz na Lord Easy wa Nako2Nako Soldiers.

Mkali wa `freestyle` Ngwair amefanya `vurugu` hata kwenye tangazo la biashara la radioni la kampuni ya huduma za simu za mkononi ambamo anasikika akipiga minato ya hatari akisema: ``Na wikiendi nzima ni full kujiachia us’pime, ni bora utembee na chaja ilimradi simu yako iszime… 12 mpaka 12 tunalonga, ni `live` bila chenga.``

Ni marejeo `ya ukweli`, kwa mujibu wake, na kwamba baada ya mashabiki kusikia `ngoma` zake mbili zilizotangulia kwa ajili albam yake mpya, hivi sasa anasambaza `Bata Kila Sehemu.`

BATA NA NGE 1982
Ikiwa ni kazi mpya aliyoirekodi katika studio ya Hammy B, wimbo wa `Bata Kila Sehemu` uliomshirikisha msanii anayechipukia J-Son, unakuja kuitangaza albam mpya ya rapa huyo iliyokamilika tayari kwa kuingizwa sokoni.

``Wimbo wa `Bata Kila Sehemu` ni zawadi kwa mashabiki wangu ambao najua walisikitika sana waliposikia nimeacha gemu,`` alisema Ngwair alipozungumza na LeteRAHA jana Jumamosi.

``Ndio wimbo wangu ambao ninausambaza hivi sasa kabla ya ujio wa albam yangu itakayoingia sokoni wakati wowote kuanzia sasa.``

Rapa huyo alisema albam yake hiyo yenye nyimbo 13 itabebwa na jina la `Nge 1982`, majina ambayo yanawakilisha nyota yake ya ‘Nge’ na mwaka aliozaliwa wa 1982.

Kwa mujibu wa Ngwair, albam hiyo imeshirikisha wakali kibao kuanzia TID, Q-Chillah, Jaymoe, Joh Makini, Mr Blue, Mandojo, Domokaya hadi mwanadada Klynn.

Pamoja na `Singida Dodoma`, `She Performs` na ‘Bata Kila Sehemu’, albam hiyo pia itakuwa na nyimbo kama `A.k.a Mimi`, `Nipeni Dili` na `Picha (sometimes ziko live, sometimes chenga-chenga)` uliorekodiwa katika studio ya Downtown Records ukimshirikisha Q-Chillah, ambaye ndiye aliyetoa wazo la `songi` lenyewe.

Ngwair alisema wimbo wa `She Performs` aliomshirikisha TID ulirekodiwa katika studio ya 69 Records ya Kinje chini ya prodyuza Mwax lakini idadi kubwa ya nyimbo amezirekodi katika studio iliyomtangaza katika gemu ya Bongo Records iliyo chini ya prodyuza P-Funk.

Alisema katika albam yake hiyo pia umo wimbo aliorekodi mwaka jana wa `07 M.A.F.I.A` ambao unabeba kifupisho cha `2007 Machizi Ambao Fani Imelala Asilia`.

“Album huenda ikawa sokoni Julai kwasababu imeshakamilika kwa kila kitu. Kwa sasa nasikilizia kidogo vitu fulani,” alisema Ngwair ambaye aliamua kukaa kando ya ‘gemu’ baada ya kukatishwa tamaa na malipo kidogo aliyopewa kutokana mauzo ya albam yake ya kwanza.

A.K.A MIMI
Albam yake hiyo ya kwanza iliyobeba jina la `Bado Nimo a.k.a Mimi`, bila ya shaka itaendelea kubaki hitoria katika gemu ya muziki wa kizazi kipya Bongo na pia kuwa miongoni mwa kumbukumbu nzuri zaidi za rapa huyo.

Ilikuwa ni albam yenye kila wimbo mtamu kuanzia `Ghetto Langu`, `Napokea Simu`, `Mikasi` `Sikiliza` aliyoimba na MwanaFA na Jaydee, hadi songi lililozua maswali kama kweli hakulikopi mahali la ``She Got A Gwan`.

Baada ya Ngwair kuwataka mashabiki wenye mashaka juu ya pini hilo kutafuta kwenye mitandao ya kompyuta kama kuna msanii duniani ameshaimba `She Got A Gwan`, tuzo ya Kilimanjaro ya Albam Bora ya Hiphop 2005 iliyotua mikononi mwake ilihitimisha mijadala juu ya wimbo huo na uwezo mkubwa kisanaa alionao rapa huyo katika gemu.

Lakini licha ya kutingisha chati zote za nyimbo bora za vituo vya radio na televisheni kwa muda mrefu, Ngwair alijikuta, kwa mujibu wake, akiambulia malipo ``yenye kukatisha tamaa`` kutoka kwa wasambazaji wa kazi za muziki nchini maarufu kama `Wadosi`.

Na Ngwair akakata tamaa kweli na kujiweka kando ya fani hiyo kujipanga kivingine kabla ya kurejea hivi sasa. Kwa spidi ile ile 120.

  • SOURCE: Lete Raha
TODAY
-----------------------------------------------
Editorial
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.