|
Watu 3 wamekamatwa kwa tuhuma za kusafirisha samaki wachanga hai
2008-05-16 15:45:07
Na Radio One Habari
Watu watatu wamekamatwa kwa tuhuma za kusafirisha samaki hai wachanga zaidi ya Laki-2 aina ya NEKE kutoka mito iliyopo Burundi na Rwanda kwa ajili ya kwenda kuwatumia kama chambo katika kuvua samaki wakubwa aina ya Sangara katika visiwa vya wilaya ya Sengerema, mkoani Mwanza.
Kaimu afisa uvuvi wa wilaya ya Chato Bwana Charles Ndibalema ameiambia Radio One kuwa watu hao watatu wamekamatwa na kikundi cha ulinzi wa rasilimali katika ziwa Victoria- BMU- kwa kushirikiana na polisi katika wilaya ya Chato mkoani Kagera.
Amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Malelemba Robert, Yahaya Joseph na Mashaka Ramadhani wakazi wa wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza.
Bwana Ndibalema amesema sheria ya uvuvi hairuhusu wavuvi kusafirisha samaki bila kibali cha uvuvi na usafirishaji kinachoonesha ubora wa samaki.
|