|
Rukwa wapongeza mpango wa shamba darasa
2008-05-11 20:01:28
Na Radio One Habari
Baadhi ya wakulima mkoani Rukwa wameupongeza mpango wa mafunzo ya shamba darasa ambao wamesema utawawezesha kuacha kilimo duni kisichokuwa na tija cha maeneo makubwa na kuchangia uharibifu mkubwa wa mazingira.
Wakizungumza na Radio One Stereo wakati wa siku ya mkulima shambani katika kata ya Msanzi kijiji cha Katuka wilaya ya Sumbawanga baadhi ya wakulima hao wamesema wana uhakika baada ya mafunzo hayo wataongeza kiasi cha mavuno na hivyo kujiinua kiuchumi.
Afisa ugani wa kata hiyo Bwana Isaack Sinkonde na mratibu wa mafunzo ya shamba darasa wa wilaya hiyo Bwana Matimba Zerubabeli wamesema mafunzo hayo yamewashirikisha wakulima 25, miongoni mwao sita ni wanawake, ambayo yamezingatia kuanzia hatua ya kuandaa shamba hadi kuvuna mazao.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga Bwana Antony Mwambene amesema kutoa ujuzi huo kwa baadhi ya wakulima kutasaidia juhudi za kukabiliana na upunfugu wa maafisa ugani ambapo waliopo 45 tu hawatoshelezi mahitaji ya vijiji 169 vya halmashauri hiyo.
|