|
Liwale yapatiwa tani 145 za chakula kutoka serikalini
2008-02-08 17:09:38
Na Radio One Habari
Serikali imeipatia wilaya ya Liwale mkoani Lindi tani 145 za chakula aina ya wanga, kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wanaokabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula wilayani humo.
Kiasi hicho cha chakula ni kati ya tani 680 zinazohitajika, zikiwemo 618 za wanga na 62 za protini, ili kutosheleza mahitaji ya watu Elfu-10 Mia Tano 69 waliokumbwa na upungufu huo wa chakula kutoka vijiji 15 vya wilaya hiyo hadi kufikia Aprili mwaka huu.
Mkuu wa wilaya ya Liwale Bibi Anna Magowa, amesema chakula hicho kitauzwa kwa waathirika kwa bei ya shilingi 50 kwa kilo na kwamba tayari wilaya hiyo imeshapatiwa shilingi milioni 33 Laki Sita na Elfu-69 kwa ajili ya kusafirishia chakula hicho kutoka
Dar es Saalam.
Mkuu huyo wa wilaya alikuwa akitoa taarifa yake kwa mkuu wa mkoa wa Lindi Bwana Saidi Meck Sadiki alipotembelea wilaya hiyo kukagua maeneo yaliyokumbwa na upungufu wa chakula.
|