|
Sh. Bilioni moja zaidi itaongezeka katika mapato yanayokusanywa na serikali kila mwezi
2006-07-21 14:45:15
Na Radio One Habari
Rais Jakaya Kikwete ameeleza kuwa kama kila mwezi shilingi Bilioni moja zaidi itaongezeka katika mapato yanayokusanywa na serikali, basi serikali itakuwa na uwezo wa kufanya mambo makubwa zaidi katika kuwajengea maisha bora Watanzania.
Alikuwa akijibu swali wakati wa mahojiano na Shirika la habari la Amerika-VOA- yaliyofanyika mjini Abuja, Nigeria ambako Rais alikuwa akishiriki katika mkutano wa saba wa Leon Sullivan.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana jijini Dar es Salaam, Mheshimiwa Kikwete amesema serikali itajenga shule nyingi zaidi, barabara zaidi, vituo vya afya na zahanati zitaongezeka na fedha nyingi zaidi zitaelekezwa kwa wananchi wa vijijini ili waweze kuboresha maisha yao.
Amesema hivi karibuni mapato ya serikali yameongezeka hadi kufikia shilingi Bilioni-200.
Rais amesema mapato ya serikali yanaweza kuchangiwa kama kutapatikana mafuta na kwamba hivi sasa kumejitokeza uwekezaji mkubwa katika utafutaji wa mafuta nchini Tanzania, hali inayoonesha kuna kila sababu ya kuamini Tanzania ina hazina kubwa ambayo bado haijagundulika.
|