|
Vyuo vya maendeleo ya wananchi kukarabatiwa
2006-07-16 19:03:05
Na Radio One Habari
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Bibi Mariam Mwafisi amesema serikali inaangalia uwezekano wa kuvifanyia ukarabati kwa awamu vyuo vyote vya maendeleo ya wananchi hapa nchini pamoja na kuvipatia nyenzo muhimu za kazi kila itakapowezekana.
Amesema kazi kubwa ya wizara yake ni kuiendeleza jamii iweze kufikia malengo yaliyokusudiwa ikiwa ni pamoja na kupambana na mila potofu zinazoweza kuzorotesha maendeleo ya wananchi.
Bibi Mwafasi alikuwa akizungumza na wafanyakazi wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Chilala kilichopo katika halmashauri ya wilaya ya Lindi pamoja na jumuiya inayokizunguka chuo hicho akiwa katika ziara yake ya siku mbili mkoani Lindi.
Chuo hicho ambacho kina uwezo wa kuchukua wanafunbzi 80 kwa wakati mmoja kwa sasa kina wanafunzi 58 tu kutokana na matatizo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukosefu wa vitendea kazi kwa wanafunzi wanapokuwa katika mazoezi ya vitendo.
|