|
Kusimamishwa mkataba kati yake na kampuni ya NET GROUP hautokani na madai
2006-07-12 15:39:14
Na Radio One Habari
Serikali imesema kusimamishwa mkataba kati yake na kampuni ya NET GROUP inayosimamia kampuni ya TANESCO hautokani na madai kwamba mkataba huo ulikuwa na hujuma bali umefikia kikomo kwa mujibu wa makubaliano yaliyokuwepo tangu awali.
Hayo yamesemwa bungeni na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, mheshimiwa Lawrence Masha alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Nzega, mheshimiwa Lucas Seleli aliyetaka kujua iwapo serikali ipo tayari kusitisha na kuangalia upya mkataba huo.
Mhe. Masha amemsema kuwa tayari serikali imetoa notisi kwa Kampuni ya Netgroup kuhusu kumalizika kwa mkataba huo.
Kuhusu mafanikio ya kampuni hiyo, mheshimiwa Masha amesema NetGroup imewezesha kuongezeka kwa nidhamu ya ulipaji Ankara za umeme, kuongezeka kwa mapato ya TANESCO kutoka shilingi Bilioni-11 kwa mwezi mwaka 2002 hadi shilingi bilioni-20 kwa mwezi , mwaka huu na kuongeza ufanisi wa upatikanaji umeme nchini kwa kununua vifaa mbalimbali vipya kwa ajili ya matengenezo na ukarabati wa vituo vya umeme.
|