14 Aug 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Kiranja afia bwawani akimkimbiza mwanafunzi
 
2008-08-14 12:32:24
Na Elisante John, PST, Singida

Kiranja wa Shule ya Msingi Kimbwi, katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Alberto John amefariki dunia wakati akimfukuza mwanafunzi mtoro ili amkamate lakini alitumbukia kwenye bwawa linalojulikana kwa jina la `Muyanji`.

Mwanafunzi huyo wa darasa la saba, kupitia Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Walioikosa (MEMKWA) alikuwa na umri wa miaka 29.

Alberto alizama kwenye bwawa hilo maarufu kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji, wakati akimfukuza ili amkamate mwenzake wanayesoma wote darasa la saba aliyejulikana kwa jina la Jerard Stephano (15).

Akielezea mkasa huo wa kusikitisha, mjumbe wa kamati ya Shule ya Msingi Kimbwi, Bw. Wilfred Said alisema kuwa, tukio hilo lilitokea siku ya Jumatatu wiki hii majira ya 9:30 alasiri.

Bw. Said alifafanua kuwa siku ya tukio mwanafunzi Jared na mwenzake mmoja walikuwa wakihojiwa na mwalimu mkuu wa shule hiyo, Bw. Doto Mangosongo, akishirikiana na mwalimu mwingine aliyetajwa kwa jina la Jafari Mumbi juu ya tabia yao ya utoro.

Alisema baada ya mahojiano hayo yaliyochukua dakika kadhaa, mwanafunzi huyo na mwenzake walitakiwa kuchapwa viboko kuhusiana na kosa la utoro wa mara kwa mara, lakini badala yake alianza kutimua mbio kukwepa adhabu hiyo.

Mjumbe huyo alilifafanua kuwa ``baada ya mwalimu mkuu kumwamuru mwalimu Mumbi awachape viboko wanafunzi hao, kabla hajaanza kutekeleza adhabu hiyo ghafla Jerard alianza kutimua mbio.

``Hapo ndipo mwalimu Mumbi alimwamuru kiranja Alberto kumkimbilia Jerard ili amkamate, lakini kutokana na uwezo mkubwa wa kukimbia alifika hadi bwawani kilomita mbili toka shuleni kisha akaanza kuogelea hadi ng`ambo ya pili, lakini marehemu alipofika katikati alizidiwa na maji baada ya kuishiwa nguvu,`` alisema Said.

Hata hivyo, Bw. Said alisema kuwa kutokana na ujasiri wa kiranja (marehemu) alipofika bwawani naye alivua kaptula yake na kumkabidhi mwenzake kisha alijitosa majini kabla ya kuzidiwa na kupoteza maisha yake.

Aidha baada ya taarifa kuwafikia wananchi wa kijiji hicho, walianza juhudi ya kutafuta mwili wa marehemu majini tangu siku ya tukio lakini hadi juzi juhudi hizo zilikuwa hazijazaa matunda.

Juzi ofisa elimu wa halmashauri ya wilaya ya Singida, Bw. Patrick Mwaluli alifika eneo la tukio na kuongoza wananchi wa kijiji hicho mchana kutwa kusaka mwili wa kiranja huyo ndani ya bwawa.

Hata hivyo, juhudi hizo zinaathiriwa kwa kiwango kikubwa na vifaa duni vya uokoaji vinavyotumiwa ambavyo ni nyavu chakavu na kamba kukatika ovyo wakati wakiwa kwenye juhudi hizo.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.