|
Serikali ihamasishe makampuni zaidi kutafuta gesi asilia
2008-05-16 10:04:07
Na Felix Andrew
Kumekuwapo na kasi ya ongezeko la utafutaji wa mafuta na gesi asilia katika mikoa ya kusini, ambayo inatakiwa iendane na wingi wa makampuni ya utafiti wa mafuta kwa lengo la kuleta ushindani. Katika makala haya Mwandishi Felix Andrew anaeleza zaidi.
Kufuatia kuongezeka kwa bei ya mafuta katika soko la dunia, kukua kwa teknolojia na mazingira mazuri ya uwekezaji, hamasa ya utafutaji mafuta hapa nchini imeongezeka.
Bei ya mafuta ya kuendeshea mitambo katika soko la dunia imekuwa inapanda kila siku, ambapo kwa sasa pipa moja la mafuta yasiyosafishwa linazidi kupanda bei.
Serikali imekuwa ikiweka mazingira mazuri ili kuvutia makampuni, ambapo kwa sasa kasi ya kutafuta mafuta katika maeneo ya kusini imeongezeka sana katika miaka ya karibuni ikilinganishwa na miaka mingine.
Tayari makampuni kadhaa yapo katika maeneo hayo yakiendelea kutafuta gesi huku mengine yakiwa tayari yameanza kuzalisha gesi. Makampuni hayo ni Ndovu Resources inayotafuta mafuta, na kampuni za Artumas na Songas tayari zimeanza kusambaza umeme wa gesi katika mikoa ya Kusini na Dar es Salaam.
Makampuni mengine matatu yalitarajiwa kusaini mkataba na serikali mwaka huu, kwa ajili ya utafutaji mafuta katika maeneo ya Ziwa Tanganyika, Bonde la Mto Ruvu na Kitalu Na. 8 katika kina kirefu baharini.
Mbali ya mafuta ya gesi kugunduliwa katika mikoa ya Kusini, gesi asilia pia imegunduliwa katika kisima cha Mkuranga, ambapo tayari serikali imeamua kuharakisha uhakiki makini wa kuwepo gesi asilia ya kutosha katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa Wizara ya Nishati na Madini mwaka 2007/08,
Takwimu za mitetemo (seismic) za kilomita 200 zitakusanywa ili kuainisha maeneo ambayo yatachimbwa visima vingine kwa ajili ya kutathmini kiasi cha gesi iliyopo.
Uchimbaji wa visima hivyo ulianza mapema mwaka huu, kutegemea matokeo ya taarifa za mitetemo ambapo Serikali itaendelea kuratibu shughuli hizo.
Katika kuendeleza juhudi hizo za kutafuta mafuta, kampuni ya Ndovu Resources tayari imeanza utafiti wa mafuta na gesi katika kisiwa cha Kiliwani kilichopo eneo la Songo Songo.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa kampuni hiyo Balozi Isaya Chialo, utafiti wa awali unaonyesha kuwa, kuna dalili ya kuwepo mafuta na gesi eneo hilo na kwamba kampuni hiyo itafanya utafiti zaidi.
Akizungumza wakati wa semina iliyoandaliwa kwa viongozi wa vijiji vilivyo ndani ya mradi huo mwaka jana, alisema kuwa kampuni imetenga fedha zitakazotumika kulipa fidia kwa wanakijiji watakaoathirika na utafiti huo.
Alisema kampuni hiyo imetengeneza miundombinu katika eneo la utafiti na kwamba wataiachia uongozi wa kijiji namna ya kuiendeleza.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Charles Gishuli, aliwaasa viongozi hao kuwaelimisha wananchi kuhusiana na umuhimu wa uwekezaji kanda ya kusini, kwani hiyo ndiyo njia pekee ya kujikomboa.
Alisema kuwa, serikali itajitahidi kuhakikisha kuwa watu wote wanalipwa fidia kwa wakati muafaka.
Hata hivyo, watalaam wa masuala ya miamba wanasema kuwa eneo la mikoa ya Kusini, lina akiba ya kutosha ya mafuta ya gesi asilia na kinachotakiwa ni kuwepo kwa miundombinu imara, itakayowezesha kusafirisha bidhaa hiyo nje ya nchi.
Tayari serikali imekwisha hakikisha kuwa umeme utakaokuwa unazalishwa katika mikoa hiyo utalinufaisha taifa na kuchangia kukua kwa uchumi.
Makamu wa Rais, Dk Ali Mohammed Shein, amekaririwa akisema katikati ya mwaka jana kuwa, serikali itahakikisha umeme wa gesi unaozalishwa mkoani Mtwara siyo tu unainufaisha mikoa ya Lindi na Mtwara, bali pia mikoa mingine nchini, ukiwemo Ruvuma, na ziada itauzwa nchi za jirani.
``Mipango ya serikali ni kwamba umeme huu wa gesi usiishie kwenye mikoa ya huku kusini tu, lazima ufike mpaka Ruvuma na mikoa mingine nchini. Kama kutakuwa na ziada, basi wenzetu wa nchi za jirani wanautaka,`` amesema Dk. Shein.
Aliyasema hayo wakati akizungumza na wazee wa kijiji cha Msimbati, mara baada ya kutembelea mradi wa uchimbaji wa gesi wa Mnazi Bay, unaoendeshwa kwa ubia baina ya kampuni ya Artumas na shirika la Uendelezaji Mafuta nchini, (TPDC).
Awali wananchi walimweleza Makamu wa Rais kwamba gesi inayochimbwa kijijini hapo, ndiyo inayotumika kuzalisha umeme unaotumika mjini Mtwara, lakini cha ajabu ni kwamba wao hawajapewa kipaumbele cha umeme huo.
Naye Meneja Utawala wa kampuni ya Ndovu Resources , Bw. Majid Kulunge, anasema utafiti wa mafuta na gesi unatarajia kuanza katika Kisiwa cha Kiliwani mwishoni mwa mwezi huu.
Anadokeza kuwa zoezi hilo linatarajiwa kuchukua miezi sita hadi mwaka mmoja, na endapo watagundua dalili za mafuta wataanza uchimbaji.
Zoezi la utafutaji i wa mafuta pia litafanywa katika vijiji au maeneo saba ambapo wanakijiji watakaothirika watalipwa fidia mara baada ya kukamilika kwa uchambuzi.
Anasema Ndovu Resources pia imepata eneo mkoani Mtwara ambapo pia wanatarajia kufanya utafiti wa mafuta.
``Utafiti wa mafuta katika mkoa wa Mtwara ulitarajiwa kuanza mwaka huu , kwani walikuwa wananasubiri ripoti kutoka kwa maafisa wa ufundi endapo kuna dalili ya kuwepo kwa mafuta``, anasema meneja huyo.
Hata kabla haujuwanufaisha ipasavyo watanzania, tayari nchi jirani zimekwisha onyesha nia ya kununua umeme wa gesi ambao umeanza kuzalishwa nchini miaka miwili iliyopita.
Nchi ya kwanza kuonyesha nia hiyo ni Kenya, ambayo mapema mwaka jana ilisema kuwa inakamilisha maandalizi ya kununua umeme wa gesi kutoka Tanzania, mwishoni mwa mwaka huu.
Hatua hiyo inafuatia Makamishna wa Nishati wa Kenya na Uganda kusifu kasi ya utafutaji gesi na mafuta nchini Tanzania, huku Kamishna wa Kenya akisema nchi yake kwa sasa inaharakisha kuboresha miundombinu yake tayari kununua umeme kutoka kampuni ya Artumas ya Tanzania.
``Mambo yakienda vizuri, Kenya itaanza kununua umeme kutoka Tanzania mwishoni mwa mwaka huu, tunachofanya kwa sasa ni kuboresha mifumo yetu, ili umeme uweze kupitishwa kirahisi kuja kwetu,`` alisema Bw. Don Riaroh ambaye ni Mkurugenzi wa Utafutaji na Uzalishaji Nishati nchini Kenya.
Juhudi hizi za Tanzania katika kutafuta mafuta na gesi zinadhihirisha kuwa, muda si mrefu Afrika Mashariki itajiunga katika familia ya nchi zinazozalisha mafuta duniani, alisema Bw. Riaroh na kuongeza kuwa amefurahishwa kipekee na kasi ya uendelezaji wa gesi ya Mnazi Bay.
Watanzania wanapaswa kujiona kuwa wana bahati kubwa kwa kufanikiwa kuzalisha umeme wao kutokana na gesi hususani wakati huu ambao upungufu wa umeme umekuwa ni tatizo sugu katika Afrika Mashariki.
Umeme ni mojawapo ya chanzo muhimu cha maendeleo ya uchumi, bila kuwepo kunaweza kuuyumbisha kwa kiasi kikubwa.
Kinachotakiwa ni kwa serikali kuweka utaratibu mzuri utakao hakikisha kuwa, kila mwananchi au taasisi wanapata huduma ya umeme kwa bei nafuu tofauti na ilivyo sasa.
Serikali katika mantiki ya kupunguza mzigo wa bei ya gesi kwa mtumiaji wa umeme, ilitoa tamko namba 246 linalohusu msamaha wa kodi, ushuru au malipo yoyote kwenye gesi asilia na miundombinu inayotumika kupitisha gesi katika Wilaya za Kilwa, Utete, Rufiji, Mkuranga, Temeke, Ilala na Kinondoni.
Kinachotakiwa ni serikali kuendelea kuratibu na kuhamasisha matumizi ya gesi asilia ili kuliepushia taifa hasara itokanayo na ununuzi wa mafuta kutoka nje ya nchi.
|