15 May 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Uchomaji moto plastiki ni tishio kwa viumbe na mazingira
 
2008-05-15 08:57:26
Na JACKSON KALINDIMYA

Tabia ya kuchoma moto mabaki ya plastiki kwa lengo la kusafisha mazingira, bila ya kujua moshi wake ni sumu ambayo huchafua, hewa, majani, udongo, maji na kuhatarisha maisha ya watu na viumbe kwa ujumla.

Mchana wa jua kali, mama Grace (sio jina lake halisi) alifagia uwanja wa nyumba yake kwa kutumia kifagio chenye mpini mrefu ili kuyaweka mazingira safi ya eneo hilo.
Mgongoni amembeba mtoto wake mdogo.

Watoto wake wengine wanacheza na watoto wenzao wa nyumba ya jirani.

Anapokamilisha zoezi hilo, anaukusanya uchafu na kwenda kuutupa kwenye jalala lililopo kando ya nyumba hiyo inayopakana na nyumba zingine.

Mama Grace anaendelea kuokota uchafu mwingine, hasa mifuko ya plastiki, chupa za plastiki, mabomba ya plastiki na takataka nyingine.

Anaokota mabaki ya ndoo za plastiki, mabomba, galoni na nyinginezo za aina hiyo kwa ajili ya kuharibu mazalia ya mbu na maficho ya wadudu wengine.

Zote anazitupa jalalani pamoja na takataka nyingine.
Hakuishia hapo.

Anakwenda ndani kuchukua chupa yenye mafuta ya taa na kuyamiminia juu ya takataka hizo na kuwasha moto.

Moto mkubwa unawaka na kusambaa jalalani. Moshi mwingi unapaa angani na kusambaa huku na huko katika eneo hilo.

Yeye amesimama kando yake akiwa ameshika fimbo ndefu.

Anazigeuzageuza taka hizo ili kuhakikisha kuwa zinateketea kabisa kwa moto ili eneo hilo liwe safi kabisa.

Mara kadhaa anakohoa na kuendelea na zoezi hilo. Utaratibu huu ameuzoea na anaufanya kila mara ikiwa pamoja na jirani zake.

Watanzania wengi wana tabia ya kuchoma moto takatakata ikiwa pamoja na zile za plastiki katika maeneo ya mijini na vijijini.

Kwa kuchukua hatua hiyo, ni kweli mazingira yao yanasafishika.Lakini bila ya kujua kuwa kumbe kuna hatari nyingine kubwa na ya kutisha zaidi kuhusu maisha yao na viumbe hai.

Wanasayansi wanasema kuwa uchomaji moto plastiki au mabaki yake ni hatari sana kwa maisha na mazingira kwa ujumla.

Plasitiki zinapochomwa hutoa sumu hatari sana aina ya dioxin.

Pia zinaweza kusababisha kemikali fulani kusambaa hewani ambazo zikivutwa zinaweza kuchangia kusababisha kansa.

Sumu hizo zinaweza kuzama ardhini, juu ya maji au kwenye mimea mbalimbali.

Kwa ujumla hatari zake ni nyingi. Sumu zinazotoka kwenye plastiki zinaathiri udongo, maji na hata kupenya kwenye chakula cha binadamu na wanyama.

Utafiti mbalimbali unabainisha kuwa sumu inayotoka katika plastiki za aina mbali zilizochomwa zikiwemo za mabaki ya makasha ya kuhifadhia kemikali na madawa ya mashambani, zinaweza kupenya kwenye mafuta ya wanyama na kisha kumrudia binadamu anapokula nyama, samaki au vyakula vingine.

Uchomaji wa takataka za plastiki, mara nyingi unafanyika kwenye mazingira ambayo ni ya karibu ya vyakula au majani ambayo baadhi yake ni mbogamboga kwa matumizi ya kila siku au mara kwa mara.

Sumu inayoganda kwenye majani hayo ambayo siyo rahisi kuiona kwa macho, binadamu huyachuma na kuyatumia kwa mboga na kisha huyala na kuingia mwilini hata kusababisha madhara makubwa.

Ni ukweli ulio wazi kuwa baadhi ya majani ni chakula cha wanyama na binadamu ambao wanasayansi wanasema kuwa sumu inayoganda kwenye majani hayo zinaweza kusababisha kansa na hata vifo.

Kwa ujumla hatari ni nyingi ambazo sio rahisi sana kuziona kwa macho na wakati mwingine madhara yake hayawezi kujitokeza mara moja.

Hujitokeza baadaye wakati tayari tatizo limekuwa kubwa na hata kuchangia kifo au vifo.

Kwa hiyo kwa namna yoyote ile, ni muhimu sana kupunguza hatari hiyo kwa kuepuka kuchoma taka hizo holela kwa lengo la kuyasafisha mazingira.

Ni muhimu sana ukaandaliwa utaratibu wa kuzikusanya takataka, kuzichambua zile za plastiki na kwenda kuzichoma au kuziangamiza kwa kutumia utaratibu maalum unaohakikiwa na watalamu husika ambao wana utaalamu na vifaa vya kufanya hivyo.

Vinginevyo takataka hizo zinatakiwa kukusanywa na kuzipeleka katika viwanda vya kuzitengeneza upya kwa mfumo mpya hata kufaa kwa matumizi mengine ambayo ni salama kiafya na kimazingira.

Ofisi ya Makamu wa Rais, kupitia Wizara ya Mazingira imekuwa ikihimiza matumizi bora na hifadhi ya mazingira kwa kuhakikisha kuwa ardhi na hewa hazichafuliwi na kuathiri maisha ya binadamu, viumbe na uoto wa asili.

Makamu wa Rais, Dk Ali Mohammed Shein mwaka juzi alipiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki yenye upana wa milimita 0.03 ili kuyanusuru mazingira.

Mifuko hiyo ambayo ilikuwa inatupwa na kuzagaa ovyo, ilikuwa inasababisha kuziba kwa mifereji ya maji, kuhatarisha maisha ya wanyama wanaokula mifuko hiyo na kuzuia usagaji wake tumboni ikiwa pamoja kushindwa kuteketea ardhini pindi yanapozikwa na hivyo kusababisha uharibifu mkubwa wa ardhi na mazingira kwa ujumla.

Uamuzi huo wa kusitisha utengenezaji na uingizaji wa mifuko ya aina hiyo, ulilenga kuokoa uharibifu zaidi wa mazingira.

Kwa hiyo, wakati utekelezaji wa amri ya serikali ya kudhibiti matumizi ya mifuko ya plastiki hiyo unaendelea ili kuhakikisha kuwa mazingira yanalindwa kutokana na uharibifu unaotishiwa na kuzaagaa kwa mifuko, ni muhimu sana jamii ikaelimishwa na kutambua hatari kubwa iliyopo hata kujiepusha na uchomaji wa plasitiki za aina yoyote ile.

Plastiki zinatofautiana ukubwa na aina ya madawa yanayotumika kuchangywa ili kuyapata katika umbo linalotakiwa la kumudu matumizi mbalimbali. Kwa hiyo kuchoma plastiki bila ya kufahamu aina ya sumu iliyomo humo ni hatari zaidi.

Ni vyema viongozi wa juu wa serikali, wabunge,vyama vya siasa, asasi za kijamii na viongozi wa ngazi na kada zote kila wanapopata nafasi kuielimisha jamii kuhusu umuhimu wa kuacha kuchoma plasitiki ili kujiokoa na hatari mbalimbali zinazoweza kutokea kwa maisha ya viumbe na binadamu.

Ni muhimu ikafahamika kuwa uchomaji moto vifaa vya plasitiki husababisha uchafuzi wa hewa na mazingira kwa ujumla.

Kwa ujumla usafishaji wa mazingira ni lengo na utaratibu mzuri sana, lakini tahadhari zote za kuhakikisha kuwa afya za watu zinalindwa na mazingira yao zichukuliwe kwa makini zaidi.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.