14 May 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Kuzomewa viongozi ni uhuru wa mawazo au demokrasia iliyopitiliza?
 
2008-05-14 10:14:40
Na Moris Lyimo

Katika siku za hivi karibuni, baadhi ya wanaharakati wamekuwa wakitoa madai kuwa kabla na baada ya uhuru, Tanzania haijawahi kuwa na `demokrasia huru` labda uhuru wa kujitawala kutokana na mfumo wa kisiasa wa nchi hiyo kuchukua nafasi kubwa katika utawala wa chama na kiserikali kwa mantiki kwamba viongozi wengi wanatokana na vyama kama ilivyo uteuzi wa Mawaziri.

Ndiyo kusema nafasi za uteuzi ni chache kulingana na katiba ya nchi, na wale wanaoteuliwa kama vile wakuu wa wilaya, mikoa, wakurugenzi wa idara mbalimbali.

Baadhi yao ni wabunge kwa maana ya wanasiasa na kwamba kwa nafasi hizo kazi kubwa wanayopewa ni kueneza sera za chama chao kwa ngazi hiyo, kusimamia na kuhamasisha maendeleo kwa mwavuli wa chama husika.

Wanasayansi wa masuala ya jamii wanasema kuwa kutokana na mfumo huo, kumekuwa na kulindana kisiasa kwa misingi ya usisi, uanachama wetu hata kama mkosaji amefanya hujuma, mfano kufuja fedha za umma ambazo zinawahusu pia wengine wenye itikadi tofauti.

Naungana na wanasayansi hao, lakini natofautiana nao baada ya kuonekana mabadiliko makubwa katika kipindi hiki cha awamu ya nne kwa sababu kama ni demorasia imeonekana kwa kiwango kikubwa bila kujali itikadi za kisiasa.

Katika awamu hii tumeshuhudia viongozi wa juu wa serikali wakikosolewa waziwazi na wanachama wenzao, jamii na vyombo vya habari bila kutetereka kwa sababu za kutetea maslahi ya umma.

Si jambo la kushangaza tena katika awamu hii kuona, Wabunge wa chama kimoja kusemana Bungeni na kumtaka kiongozi ajiuzulu ukilinganisha na awamu zilizopita ambapo Tume ya Maadili ya Viongozi ilipewa `meno` mno na kusababisha kuwepo kwa mfumo wa kulindana ambao ulitoa mwanya wa kufujwa fedha za umma.

Utangulizi huu umeandikwa kwa makusudi kabisa ukifananishwa na kile kinachosemwa kuwa Rais Mustaafu Benjamin Mkapa alizomewa Jijini Dar es Salaam hivi karibuni na baadhi ya vijana ambao waliketi pembeni mwa barabara msafara wake unapopitia.

Inadaiwa kuwa, walisikika wakimzomea kwa kumita kuwa ni ` Fisadi` na kejeli nyingine.

Bila shaka vijana hao walichukua uamuzi huo baada ya kuzagaa kwa taarifa zinazomhusisha kiongozi huyo, aliyewahi kushikilia wadhifa wa juu kitaifa kutajwa katika orodha ya mafisadi na baadhi ya mali anazomiliki, ikidaiwa pia kuwa aliwahi kufanya biashara akiwa Ikulu kwa maana wakati huo akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Binafsi naona uamuzi huo si wa kistaarabu kwa sababu haumdhalilishi ndugu Mkapa peke yake ambaye alilitumikia taifa lake kwa kadri alivyojaliwa, pia unalidhalilisha taifa hili ambalo linaaminiwa kuwa lenye amani, nidhamu na sifa zote zinazostahili binadamu kuzifanya.

Nasema hivyo kwa sababu maana ya kutetea maslahi yako haifanywi kwa mtindo huo ninaoufananisha na vurugu baada yake wangetakiwa kutumia njia ambayo isingemdhalilisha kiongozi wao huyo mstaafu.

Kwa namna yoyote, Mkapa ameifanyia kazi kubwa nchi hii ambaye historia itamtetea.Yawezekana leo hii wakawepo baadhi ya watu wakawa wakifanya kazi kubwa ya kmchafua ili wafanikishe mambo yao.Lakini ukweli utajidhirisha siku moja.

Hii ni kutokana na ukweli kuwa msingi mzuri aliouweka wa uchumi, miundo mbinu aliyoijenga ikiwemo barabara,shule,jengo la Bunge,Uwanja wa Taifa,ukarabati wa ofisi za serikali na Hosopitali za Muhimbili na kurudisha imani ya wafadhili wa nje ni miongoni mwa mambo machahe kati ya mengi aliyoyafanya kwa uzalendo wa hali ya juu.

Mimi ni miongoni mwa watu wanaokerwa na ufisadi hapa nchini, lakini zipo njia za kulalamika na siyo kuropoka hovyo, tena kwa kuvizia kando ya barabara na hivyo kushindwa kutumia demokrasia na uhuru wa kutoa mawazo kwa njia za kiusalama wa kisheria hasa kwa sababu sina hakika kwamba wana vielelezo vya dhahiri vya kumhusisha moja kwa moja na ufisadi zaidi ya kusikia kwa watu ambao haifahamiki sawasawa wana ajenda gani.

Nasisitiza tena kwa kusema kuwa, kila Mtanzania ana uhuru wa kutoa mawazo, lakini mfumo wa utoaji mawazo lazima uzingatie sheria na vielelezo pindi utakapokuwa unadaiwa kwa hoja au mawazo yenye kumshutumu au kumhusisha mtu na kashfa kama hiyo ya ufisadi. Zaidi ya hapo ni vurugu au demokrasia iliyovuka mipaka.

Kuhusu kuwa na akaunti nje ya nchi, kuna mantiki gani ya kuwa na akaunti nje ya nchi ingawaje nchi yetu inatajwa kuwa ni miongoni mwa zile zinazopiga hatua katika huduma bora za mabenki baada ya kuingia katika mfumo wa utandawazi ambapo wawekezezaji wengi wameanzisha mabenki hapa nchini ?

Maana ya kuwa na mabenki mengi ni dalili ya mwamko wa Watanzania kujiwekea akiba zao nchini na hivyo kutolazimika kuwa na akaunti nje ya nchi kama viongozi wachache wanavyofanya hivyo kwa nia ya kujilimbikiza mali kwa kificho.

Mtazamo wa baadhi ya watu kuwa na akaunti nje ya nchi unaonyesha jinsi watu hao wasivyoitakia mema nchi yetu kiuchumi.

Kwa tafsiri ya harakaharaka, kuacha huduma inayopatikana nchini mwako bila ya sababu za msingi na kukimbilia nchi za nje maana yake ni kutoiamini nchi yako.

Napenda kutumia nafasi hii kuwashawishi matajiri waweke fedha zao katika akaunti za mabenki ya ndani ili fedha hizo ziweze kusaidia maendeleo ya watu wengine.

Bila kufanya hivyo, nchi yetu itaendelea kuwa masikini kwani fedha zinazowekwa na Watanzania nchi za nje faida yake inawasaidia watu wa huko huko.

Katika nchi kama Tanzania ambayo demokrasia yake inakua hasa katika siku hizi za usoni ni wazi kwamba vitendo hivi vikiendelea vitasababisha mgawanyo wa makundi katika jamii.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.