13 May 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Vyombo vya habari viimarishe ujasiri wa kuielimisha jamii
 
2008-05-13 08:52:56
Na PETER TINDWA

Rais wa zamani wa Marekani, hayati Abraham Lincoln, aliwahi kusema kwamba demokrasia ni utawala wa wananchi.

Usemi huu unahitaji kuwepo kwa jamii inayoelewa vyema demokrasia ambapo kazi ya kuelimisha ni jukumu la waandishi wa habari.

Uhuru wa vyombo vya habari kwa mujibu wa Shirikisho la Waandishi wa Habari la Kimataifa (IFJ) ni hali ya kutokuwepo kwa vikwazo vinavyoweza kuwazuia waandishi wa habari, wahariri na wachapishaji kutangaza au kusambaza ukweli pamoja na maoni ambayo bila kufahamika kwa wananchi yatawafanya washindwe kufanya maamuzi bora.

Hivi karibuni kumekuwepo malalamiko kutoka kwa baadhi ya watu, wakiwamo viongozi wa serikali wakidai kuwa habari za ufisadi zimepewa kipaumbele mno kuliko habari nyingine za maendeleo.

``Ninyi waandishi wa habari nawashangaa sana. Mmeng`ang`ania habari za Richmond, EPA na Benki Kuu huku mkiziacha habari za maendeleo,``Waziri wa Kilimo na Chakula, Steven Wassira,`` alisema.

Walalamikaji wanapaswa kuzingatia kuwa mabilioni ya Shilingi yanayopotea kijanjajanja yanawanyima maendeleo mamilioni ya wananchi. Wananchi hao hao ndio wapigakura.

Hivyo, ni haki yao ya msingi na kikatiba pamoja na kidemokrasia kuelimishwa ukweli juu ya upotevu wa fedha za nchi yao.

Vyombo vya habari vinawaelimisha ukweli wa sakata zote hizo ili watakapohitajika kutoa maamuzi sahihi kuhusu serikali yao watauzingatia ukweli walioupata kupitia vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi.

Ili kuhakikisha uhuru wa vyombo vya habari unakuwepo, vyama vya waandishi wa habari ni lazima vikatae mbinu zozote zenye lengo la kuvibana vyombo hivyo iwe kwa njia ya kuchuja habari au hata kwa kutuhumiwa kuwa vyombo vyao huandika au hutangaza habari fulani tu na zingine huziacha.

``Mbinu za kuingilia uhuru wa vyombo vya habari zinaweza kuwa kama zilivyotajwa au kwa njia ya matangazo na pia kwa shinikizo la kibiashara,`` IFJ inasema.

Tishio dhidi ya vyombo vya habari si uchujaji wa habari wa moja kwa moja. Bali uchujaji unaofanywa na wahariri pamoja na waandishi wenyewe.

``Vyombo vya habari na waandishi wao wana nafasi muhimu katika mfumo wa vyama vingi. Lakini wanaweza kuwa na nafasi hiyo iwapo tu watafuata maadili ya taaluma yao na kuwajibika kwa kazi yao,`` Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, alisema mwaka 1996.

Naye Rais, Jakaya Kikwete, akifungua rasmi kituo cha TBC1 jijini Dar es Salaam hivi karibuni alisisitiza kwamba serikali yake itaendelea kuwaheshimu waandishi wa habari.

Hata hivyo, alisema kuwa ni muhimu kwa waandishi wa habari kuwajibika kwa taaluma yao.

Msisitizo unaowekwa wa waandishi wa habari kuzingatia maadili ya taaluma yao unawafanya waandishi wa habari kujitahidi ili kujiepusha kuingia katika mazingira ambayo yatawaweka katika nafasi ya kubanwa na serikali pamoja na taasisi zake.

Mara kwa mara vyombo vya habari vimeaswa kuimarisha ushirikiano na mshikamano ili kulinda na kuimarisha taaluma ya habari.

Chuki ikiachwa iendelee miongoni mwa vyombo vya habari matokeo yake si mengine bali kudharauliwa na wananchi.

Ni wazi kuwa upendeleo kwenye vyombo vya habari upo kila wakati. Lakini unajitokeza sana wakati wa uchaguzi.

Kukosekana kwa habari fulani katika magazeti, redio au luninga kwaweza kutafsiriwa kuwa ni upendeleo kwa baadhi ya wanasiasa na pia makundi fulani.

Lakini ifahamike wazi kuwa makosa ya namna hii yanaweza kutokea kutokana na shinikizo pamoja na ufinyu wa muda, ambapo hoja za kitaaluma zinaweza kufumbiwa macho.

Kwa ujumla waandishi wa habari wanapaswa kujitahidi kuepuka upendeleo ili upangaji wa habari uzingatie uzito wa habari yenyewe.

Maoni ya wahariri hayapaswi kuingilia upangaji mzima wa habari jambo ambalo waandishi wamekuwa wakiliheshimu. Hata hivyo, ni vigumu kwa watu walio nje ya taaluma ya uandishi wa habari kuamini jambo hili.

Ndiyo maana shutuma juu ya upendeleo kwa misingi ya kisiasa zinakuwa rahisi kuzitoa lakini mara nyingi ni vigumu kuzikanusha.

Mifano ya kuficha ukweli au kupotosha na kutotoa uzito kwa habari za kisiasa imekuwa ikitokea hususan nyakati za uchaguzi unaohusisha vyama vingi hapa nchini tangu mwaka 1995, 2000 na 2005.

Wasomaji, wasikilizaji na watazamaji wamekuwa wakisusia ama kutilia mashaka habari zitolewazo na baadhi ya vyombo vya habari.

Upendeleo wa makusudi wa kiwango kidogo na uliovuka mpaka ni matokeo ya uamuzi wa makusudi wa mwandishi wa habari, mhariri ama mwenye kumiliki chombo cha habari kutokana na yeye mwenyewe kuwa mshabiki wa chama fulani kuliko kupitiwa.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.