|
Udhibiti wa vyeti bandia uimarishwe
2008-05-13 08:50:46
Na Mhariri
Katika miaka ya hivi karibuni kushamiri kwa mfumuko mkubwa wa vyeti feki kwenye taasisi mbalimbali za umma na vyuo vitoavyo elimu ya juu limekuwa ni tatizo ambalo tunaweza kulilinganisha na `donda ndugu`.
Tumesikia wiki iliyopita jinsi serikali ilivyolazimika kuwazuia watahiniwa 64 kufanya mitihani yao ya kufuzu kozi ya ualimu daraja la tatu kutoka vyuo vitatu binafsi mkoani Tanga.
Ilibainika kwamba, watahiniwa hao hawakuwa na stahili za kufanya mitihani hiyo ya mwisho kufuatia kukosa sifa zinazohitajika, kubwa zaidi likiwa ni kuwa na vyeti feki.
Tumelazimika kulizunguzia suala hili leo kutokana na jinsi tatizo la vyeti vya kughushi linavyozidi kukua siku hadi siku, huku juhudi zinazofanywa kulidhibiti zikionekana kuwa hafifu.
Miongoni mwa athari za watu wanaotumia vyeti feki ni taifa kujikuta likiwa na watumishi wasiokidhi viwango vinavyostahili (vihiyo), na hivyo kuathiri utendaji wa sehemu husika.
Tumepata kusikia taarifa za baadhi ya taasisi za umma kuwaajiri viongozi katika idara nyeti kama za fedha na hata hospitalini huku watumishi hao wakiwa na vyeti bandia.
Hivi sasa tumeanza kusikia baadhi ya Watanzania tena wenye nyadhifa nzito wakipata shahada za juu kutoka vyuo vya nje katika vipindi vifupi ambavyo vinatia mashaka.
Imefikia kipindi ambapo watu wanapata mashaka kuona shahada za elimu au taaluma mbalimbali zikipatikana kirahisi kama vile mtu anavyonunua mitumba kutoka kwa wamachinga.
Sisi tunaamini kwamba, kitendo cha kughushi nyaraka, ikiwa ni pamoja na vyeti vya taaluma ni kosa la jinai ambalo wahusika hustahili kufikishwa mbele ya sheria mahakamani.
Katika hali ya kushangaza, watuhumiwa wa kughushi vyeti, kama ilivyotokea katika vyuo hivyo vya ualimu, huishia kuachishwa masomo au kufutiwa matokeo, huku kiini hasa cha wao kupata vyeti hivyo bandia kikiwa hakijawekwa hadharani.
Tunadhani sasa serikali na mamlaka husika zinahitajika kubadilika, ambapo wanaokamatwa na vyeti bandia wanatakiwa kusaidia upelelezi wa kipolisi ili kuweza kuwabaini wanaovitengeneza.
Ni pale tu ambapo wanaohusika na utengenezaji wa vyeti bandia watatiwa mbaroni, kufikishwa mahakamani na kupewa adhabu kali za vifungo jela, ndipo ambapo Tanzania inaweza kupunguza uhalifu huu.
Tufikie mahali tukajiuliza, ni kiasi gani taifa linaathirika kuwa na `vihiyo` ambao hukabidhiwa madaraka yenye dhamana, tofauti na viwango vya elimu walivyonavyo?
Vyeti bandia siyo tu huwaaibisha wanaovimiliki, bali pia hata vyuo vinavyobainika kuwapokea wanafunzi wanaosajiliwa kujiunga na masomo kwa kutumia vyeti bandia.
Tungependekeza serikali iangalie uwezekano wa kusambaza vifaa vya kisasa vitakavyoweza kubaini vyeti bandia vya elimu na hapohapo kila taasisi kufuatilia kwa makini uhalisi wa vyeti vya watumishi wake kabla ya ajira ili kuweza kuzuia athari za muda mrefu.
|