|
Angola kuja kucheza na Stars
2008-05-13 08:49:07
By Somoe Ng\'itu
Timu ya soka ya taifa, Taifa Stars, inatarajia kucheza mechi ya kirafiki ya kimataifa na timu ya Angola hapo Mei 24 ikiwa ni siku inayotambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Soka, FIFA.
Kwa mujibu wa habari zilizopatikana jijini Dar es Salaam zinasema kuwa timu hiyo inatarajiwa kuwasili nchini ikiwa na wachezaji wake wote wa kulipwa na taratibu za kuileta zimefikia katika hatua za mwisho.
Chanzo hicho kilisema kuwa mawasiliano ya kuileta timu hiyo yamefanyika mapema na kuongeza kuwa timu hiyo itawasili nchini kwa gharama za Shirikisho la Soka Tanzania, TFF.
Kiliongeza kuwa mechi hiyo ni maalumu kwa kuiandaa Stars dhidi ya mechi yake na Mauritius iliyopangwa kufanyika Mei 31 kwenye Uwanja Mpya wa Kisasa uliopo jijini Dar es Salaam.
``Mara baada ya kutoka Uganda, Stars itacheza na Angola Mei 24 mchezo ambao ni kwa ajili ya kujiandaa na mechi ya Mauritius,`` kilisema chanzo hicho.
Hatahivyo, Katibu Mkuu wa TFF, Fredrick Mwakalebela jana alishindwa kuthibitisha kuwa Angola watakuja kucheza na Stars na kusema kuwa mpaka jana mchana hakuna nchi ambayo imekubali maombi waliyotuma ya kuja nchini kucheza mechi ya kirafiki.
Mwakalebela pia alikataa kutaja majina ya nchi ambazo wameziomba kuja nchini kucheza na Stars na kuongeza kuwa pia hakuna nchi ambayo imetuma maombi ya kutaka kujipima na timu yetu inayonolewa na kocha kutoka Brazil, Marcio Maximo.
Stars endapo itapata timu ya kucheza nayo itakuwa ni nafasi pekee ya kupima kikosi chake kabla ya kukutana na Mauritius hapo Mei 31 ikiwa ni mchezo wa kwanza wa kuwania kufuzu kucheza fainali za mashindano ya Kombe la Dunia na Kombe la Mataifa ya Afrika za mwaka 2010.
Katika kuhakikisha kuwa Stars inajiandaa vizuri na mashindano hayo ya kimataifa, TFF iliialika Msumbiji mwezi Machi kuja kucheza lakini ilishindikana kufanyika kwa mchezo huo kufuatia kujaa maji kwenye Uwanja wa Taifa ambao umewekwa nyasi bandia na shirikisho hilo kuingia hasara.
Stars sasa iko kambini kujiandaa na mechi yake ya marudiano dhidi ya Uganda, The Cranes itakayofanyika Kampala Jumamosi huku ikiwa katika nafasi nzuri baada ya kushinda mabao 2-0 katika mchezo wa kwanza uliofanyika jijini Mwanza wiki iliyopita.
|