|
Prisons yamnyatia Yondani
2008-05-13 08:48:16
By Jimmy Charles
Beki wa Simba na timu ya taifa, Taifa Stars, Kelvin Yondani amegeuka kuwa lulu baada ya wawakilishi wa Tanzania katika mashindano ya Kombe la Shirikisho, Prisons ya Mbeya nayo kutangaza kumtaka mchezaji huyo kwa ajili ya kuimarisha kikosi chao.
Mbali ya Prisons timu nyingine inayoonekana kumuhitaji mchezaji huyo ni mabingwa wa soka hapa nchini na mabingwa wa soka nchini, Yanga.
Akizungumza jijini jana, Kocha wa Prisons, Juma Mwambusi alisema katika kuhakikisha anakiimarisha kikosi chake amepanga mikakati ya kuongeza baadhi ya wachezaji wenye uzoefu na michuano ya kimataifa.
``Nataka kuimarisha kikosi changu, unajua unapoongelea michuano ya Kombe la Shirikisho tambua unaongelea michuano mikubwa barani Afrika, sasa ni lazima tuimarishe kikosi kwa kusajili wachezaji wenye uzoefu ili kushindana,``alisema Mwambusi.
Alisema mmoja wa wachezaji wazoefu anaowahitaji kwenye kikosi chake ni Yondani, ambaye amecheza zaidi ya mara moja michuano ya kimataifa, ambapo kwa kushirikiana na wenzake waliopo kwenye kikosi hicho kwa sasa ataisaidia timu.
Aidha, Mwambusi alisema mbali ya kumuhitaji Yondani pia anahitaji kumuongeza mlinda mlango mwenye uzoefu, walinzi wa pembeni pamoja na mchezaji mmoja wa kiungo, ambaye atakuwa na uwezo wa kugawa mipira kwa kasi ili kutafuta mabao.
Kwa upande mwingine Mwambusi, alisema hatakuwa na wasiwasi kama beki wake wa pembeni, Stephen Mwasika atakubali kuondoka kwenye kikosi hicho na kuelekea Yanga kama taratibu za uhamisho zitafuatwa.
``Binafsi sitaweza kumzuia ingawa ni mchezaji muhimu kwenye kikosi changu, pengine atakuwa ameangalia maslahi zaidi hivyo litakuwa ni jukumu lake kubaki Prisons au kwenda anakohitajika kama taratibu zote zitafuatwa na yeye mwenyewe atakuwa radhi,``aliongeza Mwambusi.
Hata hivyo tayari uongozi wa Simba ulikwisha sema kuwa hawatakuwa tayari kumuachia mchezaji wao huyo aondoke kwenye timu hiyo, ambapo tayari wameshaingia nae mkataba wa kuitumikia klabu hiyo kwa msimu ujao.
|