|
Msongamano huu wa magari unaweza kuepukwa D’salaam
2008-05-12 08:56:46
Na Mhariri
Msongamano wa magari katika jiji la Dar es Salaam, ni kero ambayo imekuwa ikiwaumiza vichwa wengi kutokana na kuongezeka siku hadi siku, huku mamlaka husika zikiwa kama hazijui zifanye nini.
Msongamano wa magari una madhara mengi, ikiwa ni pamoja na kuzorotesha uchumi wetu kutokana na watu kuchelewa makazini ama hata majumbani kupumzika ili kesho yake waamke mapema na nguvu, ari na kasi mpya.
Kabla hajajiuzulu, aliyekuwa Waziri Mkuu, Bw. Edward Lowassa, alijaribu kulivalia njuga suala hilo kwa kuanzisha utaratibu wa njia tatu, zoezi ambao bila shaka halijafanyiwa tathmini kubwa kuona matokeo yake.
Kinachofahamika kwa haraka haraka ni kwamba angalau zoezi hilo limesaidia kidogo kupunguza adha za msongamano katika baadhi ya barabara jijini Dar es Salaam, ingawa pia inaelezwa kuwa limechangia ajali kadhaa, hususan kwa waenda kwa miguu.
Hata hivyo, baadhi ya watu wanaamini kwamba hilo la ajali linataka tu elimu kubwa, ikiwezekana wahusika wanunue vipindi kwenye vyombo vya habari na kuwatangazia wananchi.
Katika kupunguza misongamano, ilikuwa inapendekezwa kwamba baadhi ya barabara za mitaani ziboreshwe ili madereva wapitie huko badala ya kutegemea barabara kuu.
Kwa mfano, watu wanaotokea maeneo ya Manzese kwenda Barabara ya Mandela, hawana haja ya kuja mpaka Ubungo, kama barabara inayopitia Chuo cha Usafirishaji hadi Ubungo Maziwa itatenegenezwa vyema.
Hilo tuliona linaanza kushughulikwa na wahusika na bila shaka mvua zinazoendelea kunyesha ndizo zimewazuia.
Hata hivyo, tumegundua kwamba foleni nyingine zingeweza kuepukwa kama barabara zingewekewa taa za kuongozea magari ama vituo vya daladala fulani kuondolewa mahala vilipo sasa.
Mfano mzuri ni eneo la Buguruni Chama. Eneo hilo mara nyingi huwa na foleni, hususan usiku, ambazo sisi tunaona ni za kujitakia.
Zamani kulikuwa na taa za kuongezea magari, lakini hatujui kwa nini ziliondolewa na kwa nini hawahusika hawajaona umuhimu wa kuzirudisha.
Pili, kituo cha daladala cha Chama kilichoko nyuma ya shule ya Msingi ya Buguruni, kinachangia sana msongamano katika eneo hilo.
Kituo hicho, kingewezwa kusogezwa mbele kidogo, kabla ya kufika Relini, na kuna sehemu ya kutosha upande wa kushoto.
Kama hilo lingefanyika, bila shaka msongamano ungepungua.
Kuna eneo la Sokota, Temeke, ambalo pia huwa na msongamano mkubwa wa magari.
Lakini sababu kubwa ya msongamano hapo ni ubovu wa barabara.
Wakati fulani mwanzoni mwa mwaka huu tuliona barabara hiyo ikufungwa, tena kwa muda mrefu, hadi magari kulazimika kupita katika kituo cha mafuta cha eneo hilo tukiamini kwamba ilikuwa inatengenezwa.
Lakini cha kushangaza ni kwamba imefunguliwa hivi sasa lakini mashimo ndio kama vile yamezidi. Hatuamini kama Halmashauri ya Manispaa ya Temeke haina uwezo wa kifedha wa kuziba mashimo katika barabara hiyo.
Maeneo tuliyoyataja, Buguruni na Sokota, ni mfano tu wa maeneo mengi katika jiji la Dar es Salaam, ikiwemo Barabara ya Mandela ambayo tukiyashughulikia yatasaidia sana kupunguza msongamano wa magari.
|