|
Kinondoni, Mara zasonga mbele
2008-05-12 08:55:25
By Mwandishi Wetu
Timu za Kinondoni na Mara jana zilisonga mbele katika michuano ya soka ya Safari Lager Taifa Cup inayoendelea, jijini, Dar es Salaam.
Timu hizo mbili hizo sasa zitavaana katika hatua ya pili ya mashindano hayo.
Kinondoni iliweza kutinga katika hatua hiyo baada ya kuilaza timu ya Shinyanga, Ingembensabo 2-1 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Taifa, jijini, Dar es Salaam.
Kinondoni ilianza mchezo huo kwa kishindo na kuweza kujipatia bao mapema katika dakika ya kwanza lililozamishwa na Juhudi Samwel.
Juhudi aliweza kupachika bao la pili tena katika dakika ya 60 wakati bao la kufutia machozi la Ingembensabo lilizamishwa kimiani na Ramadhan Sanga katika dakika ya 80.
Katika mchezo wa pili ulioanza saa 10 jioni, Mara iliiliza Singida, Kindai Shooting Stars 2-1, ambapo Athumani Matutu aliifungia Mara bao la kwanza katika dakika ya saba wakati lile la pili lilifungwa na Geoffrey Rwegasira katika dakika ya 82.
George John ndio alizamisha bao la kufutia machozi la Kindai katika dakika ya 87 kwa mpira wa adhabu. Wakati huo huo, Kamati ya mashindano ya TFF imeipa ushindi wa mezani timu ya mkoa wa Mbeya, Mapinduzi dhidi ya Temeke.
Mbeya ilipinga ushindi wa juzi wa Temeke kutokana na kuwachezesha wachezaji wawili wasiokuwa halali, Sammy Kessy na Rashid Gumbo.
Afisa Habari wa TFF, Florian Kaijage alisema kuwa kamati hiyo ilifikia maamuzi hayo baada ya viongozi wa soka wa Temeke kushindwa kuwasilisha utetezi wao.
Kaijage, alieleza, hata hivyo, kamati ilibaini wachezaji hao walikuwa Oman na walirejea nchini kucheza katika ligi ya Temeke bila ya uhamisho wa kimataifa (ITC).
Mashindano hayo yanaendelea leo kwa mechi moja tu kati ya Arusha, Mount Meru Warriors dhidi ya Iringa, Ilulu Stars.
|