|
Wadau waichagia Kinondoni Sh. Milioni 1.3
2008-05-12 08:53:54
By Abdul Mitumba
Timu ya soka ya mkoa wa Kinondoni jana ilipewa kitita cha Sh. milioni 1.3 na wadau mbalimbali wa mchezo huo katika mkoa wao ili kuongeza hamasa na jitihada katika mchezo wake wa kwanza dhidi ya Shinyanga `Igembensabo` kwenye mashindano ya Safari Lager Taifa Cup yanayoendelea kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Kati ya fedha hizo, Sh. 500,000 zimetolewa na mwanamichezo, Alex Massawe ambaye alimkabidhi mkuu wa wilaya hiyo ambaye pia ni mlezi wa timu, Kanali Fabian Massawe.
Akizungumza wakati wa kukabidhi hundi ya fedha hizo, Alex alisema amefarijika kuona Kinondoni imepewa hadhi ya mkoa na kushiriki kwa mara ya kwanza katika mashindano hayo.
Alisema amehamasika zaidi na kuchangia fedha hizo baada ya kubaini kuwa timu hiyo inaundwa na wachezaji chipukizi wasio na majina makubwa na hata ikifungwa bado atakuwa na imani nayo.
``Hatua ya Kinondoni ni tofauti kabisa na majirani zetu ambao wameamua kukusanya nyota wote kutoka Simba, Yanga na Ashati kujaza katika timu zao,`` alisema Alex.
Kinondoni na Igembensabo zilitarajiwa kumenyana jana mchana katika mchezo wa kwanza na baadaye kufuatiwa na mechi kati ya Mara na Singida.
Akipokea hundi hiyo, mlezi wa timu hiyo alisema timu yake inahitaji misaada zaidi kwa sababu ana uhakika itasonga mbele licha ya kuundwa na wachezaji chipukizi.
Alisema pia wamepokea Sh. 800,000 kutoka kwa wadau mbalimbali ambao hawakutaka kutajwa majina yao ili kusaidia jitihada za kuwezesha timu inasonga mbele.
|