|
Pemba wataka kujitenga
2008-05-11 11:58:19
Na Mwandishi wetu, Pemba
Wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF) Kisiwani Pemba, wameendeleza tishio la kutaka kujitenga na Unguja, ikiwa ni shinikizo la kusainiwa kwa makubaliano ya muafaka kati ya chama hicho na Chama cha Mapinduzi (CCM).
Wakiandamana katika barabara za Chake Chake, kupitia barabara ya Macho Manne kuelekea viwanja vya Gombani ya Kale, ambako viongozi wa juu wa CUF walihutubia, wafuasi hao walikuwa wakiimba kuwa hawataki muafaka, hawataki Serikali ya Mseto Zanzibar na kwamba wanataka Pemba iwe huru kuendesha mambo yake.
Aidha, wametangaza mgomo wa kusafirisha mazao ya chakula kwenda Unguja. Pemba inaaminika kuwa eneo kuu la uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara, visiwani humo.
Kauli hizo zimo katika risala ya wafuasi hao, iliyosomwa na Bi. Rizik Omar, baada ya maandamano yaliyofanyika jana mjini hapa.
Maandamano hayo ambayo ni mfululizo wa maandamano yaliyopangwa kufanywa na CUF kwa nyakati tofauti nchi nzima, yalianzia Macho Manne hadi Gombani, na kupokewa na Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba.
Bi. Omar, alisema mkazi yeyote wa Pemba atayekiuka tamko hilo, atachukuliwa hatua ya kutengwa, kwa vile atakuwa hana uchungu na kile walichokiita kuwa madhila wanayofanyiwa (wakazi wa Pemba) na serikali yao.
Kisiwa cha Unguja kinategemea zaidi ya thuluthi moja ya mazao ya chakula na matunda kama ndizi, muhogo, viazi, embe na mabungo kutoka Pemba.
``Sio ruhusa kusafirisha hata pilipili kwenda Unguja,``alisema Bi. Omar huku akishangiliwa na maelfu ya watu waliojitokeza kushiriki maandamano hayo.
Aidha, wakazi wa kisiwa hicho, wametakiwa wasipande meli za Mv Maendeleo na Mv Mapinduzi, zinazomilikiwa na serikali, ili kuathiri mapato ya vyombo hivyo.
Makamu Mwenyekiti wa CUF, Bw. Machano Khamis, alisema kwa kuwa uamuzi wa mgomo ni msimamo wa wanachama, CUF itawaunga mkono kwa kuwa ni moja ya njia za kuhakikisha haki inapatikana.
Alisema pamoja na kuwa uamuzi huo utamuathiri na yeye kwa vile anaishi Unguja, lakini yupo tayari kufa kutokana na njaa, alimradi haki ya wananchi wa Zanzibar ipatikane.
Naye Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, alisisitiza kuwa CUF imeshafunga mjadala wa mazungumzo ya muafaka, na haipo tayari kurejea kwenye mazungumzo na Katibu Mkuu wa CCM, Bw. Yusuf Makamba.
Alisema hivi sasa CUF inamsihi Rais Jakaya Kikwete, kumkutanisha (Maalim Seif) na Rais Amani Abeid Karume.
``Ni kikao hicho ndicho kitakachokuwa na uwezo wa kutatua tatizo la Zanzibar na si kuendelea na mzaha wa kuwa na kikao na Makamba,`` alisema.
Maalim Seif, alisema katika utatuzi wa migogoro duniani zipo njia tatu za kidikteta, kura ya maoni na mazungumzo.
``Panapotumika moja kati ya hizo njia tatu, basi nyingine zinakufa moja kwa moja na hazifai tena. Lakini kinachofanywa na CCM hapa ni usanii ambao hauonekani pengine duniani,``alisema.
Kwa upande wake, Profesa Lipumba, pamoja na kusisitiza kusainiwa kwa muafaka, alilaani kitendo kilichofanywa na viongozi wa CCM mkoani Shinyanga, kumpa mapokezi aliyekuwa Waziri wa Miundombinu, Bw. Andrew Chenge.
``Kitendo cha kumpokea Chenge kwa furaha ya nyama choma na pombe, ni kuikejeli misingi ya utawala bora na kuidharau ahadi ya Rais Jakaya Kikwete kutaka kupambana na mafisadi,`` alisema.
Mapema, wanachama wa CUF waliandamana wakiwa wamebeba mabango yenye ujumbe kama : Comoro na Kenya ni kwa wenzako…Zanzibar ni kwako; CCM msifanye usanii katika mazungumzo, wekeni mbele maslahi ya Taifa, Zanzibar ni ya Wazanzibari na Zanzibar ni sehemu ya Watanzania.
|