11 May 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Mwili wa Mchungaji wa KKKT watambuliwa
 
2008-05-11 11:56:29
Na Fitina Haule, PST, Morogoro

Mwili wa Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Morogoro, Daniel Langwa (25), aliyefariki kwenye ajali ya basi iliyotokea juzi mkoani, hapa umetambuliwa.

Pamoja naye, hadi jana miili mingine mitano kati ya abiria 12 waliofariki dunia juzi katika ajali ya basi la Al-Hushoom ilikuwa imetambuliwa.

Marehemu Langwa aliyekuwa akiishi Maguha wilayani Kilosa, mwili wake ulishachukuliwa na jamaa kwa ajili ya mazishi.

Mchungaji huyo na wasafiri wenzake waliokuwa wakitoka Morogoro kuelekea Dodoma walipoteza maisha na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya basi lao kugongana na lori eneo la Kiegeya mkoani hapa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro Bw. Thobias Andengenye, alisema marehemu wengine watano walitambuliwa siku ya tukio ambao ni watawa wawili wa shirika la Carmelite la Kanisa Katoliki Kihonda.

Marehemu hao ni Renatha Joseph na Anitha Bay ambao miili yao ilisafirishwa jana kwenda Dar es Salaam.

Aliwataja wengine kuwa ni dereva wa basi hilo Thomas Magosha (39) mkazi wa Chamwino, Khalid Maalim, aliyekuwa kondakta na Rehema Mzuwanda wote wakazi wa Manispaa ya Morogoro.

Alisema maiti sita hawajatambuliwa ambao ni mwanamke mmoja na mtoto wa kiume mwenye umri kati ya miaka minne na mitano na wanaume wanne na miili yao imehifadhiwa katika katika hospitali ya mkoa wa Morogoro.

Alisema chanzo cha ajali ni lori namba T 188 AGF kulazimisha kulipita loli jingine namba T 748 ATE lenye trela namba 446 ADU lililokuwa mbele yake.

Dereva wa lori hilo ghafla aliona basi hilo mbele na aliporudi kwenye upande wake trela lenye namba T230 ACR lilikatika na kuziba barabara na kulazimisha basi hilo kuligonga na kupinduka mara kadhaa likitumbukia bondeni.

Alisema abiria 32 walijeruhiwa katika ajali hiyo ambapo 29 kati yao walilazwa na wengine walitibiwa na kuruhusiwa na hadi sasa majeruhi 20 wapo katika hospitali ya misheni ya Berega iliyopo Gairo wilayani Kilosa.

Majeruhi wengine tisa walilazimika kupelekwa katika hospitali ya Mkoa Morogoro kutokana na hali zao kuwa mbaya.

Majeruhi kwa mujibu wa Kamanda ni Kidamani Kicheloda (Sangasanga- Mvomero), Francis Chingora(Iringa), Nissan Hoiya (Morogoro), Abdul Rashid (Dumila) , Pheres Robert (Morogoro), Nasibu Mruge (Morogoro), Mali Ngumo (Kilosa) na Wistan Amos mkazi wa Mtumbatu Kilosa.

Wengine ni Mshobe Mputa (Dumila), Athuman Mohamed( Mvomero), Jesward Mwanja (Morogoro), Ramadhani Ally (Kibati Mvomero), Bushiri Jumanne (Kihonda), Havin Chongora(Ilonda), Debora Msanya (Iringa), Jane William na Baraka Isaya wa Dumila.
Ester Sabanga (Mkundi) na Charles Kalekwa (Morogoro).

Hali za majeruhi waliolazwa hospitalini Berega na ile mkoa zinaendelea vizuri.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.