11 May 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Meya adaiwa kumnyima diwani fedha za kutengenezea barabara
 
2008-05-11 11:54:44
Na Thobias Mwanakatwe, PST Mbeya.

Barabara zilizopo katika Halmashauri ya jiji la Mbeya, hazijatengenezwa kwa muda mrefu kwa kile kinachodaiwa kuwa ni kutokana na mvutano kati ya Meya na Diwani.

Imeelezwa kuwa, Meya wa jiji la Mbeya, Bw. Athanas Kapunga hatoi mgawo wa fedha za kutengeneza barabara kwenye kata ya diwani huyo kwa sababu hawaelewani.

Hayo yalibainishwa na wajumbe wa kikao cha Bodi ya Barabara ya Mkoa kilichofanyika jijini hapa ambacho kilikuwa kikijadili hali ya barabara za mkoa wa Mbeya.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Bw. John Mwakipesile akizungumza katika kikao hicho, alisema wananchi wa jiji la Mbeya, wamekuwa wakilalamikia ubovu wa barabara hali ambayo inaleta kero kwao.

``Suala la ubovu wa barabara kwenye Halmashauri ya jiji la Mbeya, linalalamikiwa sana pia na wananchi, ambapo wanadai diwani asiyekuwa rafiki wa Meya wa Jiji, hapati fedha za kujengea barabara kwenye kata yake,`` alisema Mkuu wa Mkoa.

Hatua ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya kueleza bayana tatizo la ubovu wa barabara lilifuatia baada ya Mbunge wa Viti Maalum, Bi. Flrolence Kyendesya na Mbunge wa Mjini, Bw. Benson Mpesya kuitupia lawama halmashauri ya jiji la Mbeya kwa kutokuwa makini katika suala la kutengeneza barabara.

Mbunge wa Viti Maalum, Bi. Kyendesya alisema Halmashauri ya Jiji la Mbeya haiko makini katika kutengeneza barabara ambapo alitoa mfano wa barabara ya Ituha ambayo ni mbovu kupindukia na kuleta kero kubwa kwa wananchi wa eneo hilo.

Alisema wananchi ambao maeneo yao barabara ni mbovu wamekuwa wakilalamikia hali hiyo kwa kupitia kwa viongozi wao na pengine kuwasiliana na viongozi wa jiji bila mafanikio hatua ambayo imefanya wananchi kutokuwa na imani tena na halmashauri hiyo.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe Bw.John Mwankenja alisema lawama zinatolewa na wabunge dhidi ya halmashauri ya jiji la Mbeya zinatokana na halmashauri hiyo kutowashirikisha katika mipango mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya ujenzi wa barabara.

Bw. Mwankenja alisema kufuatia hali hiyo halmashauri ya jiji la Mbeya ibadilike kwa kuhakikisha inapoitisha vikao mbalimbali vya kujadili mipango ya maendeleo wanaitwa wabunge badala ya kuitisha vikao hivyo kisiri siri.

Meya wa Jiji la Mbeya Bw.Athanas Kapunga, akijibu malalamiko hayo alimhakikishia Mkuu wa Mkoa pamoja na wajumbe waliokuwepo kwenye kikao hicho kwamba halmashauri itajitahidi kuhakikisha barabara zinazolalamikiwa na wananchi zinatengenezwa haraka mwaka huu.

Bw. Kapunga akielezea kuhusu madai ya kwamba diwani asiyekuwa rafiki yake hapewi mgawo wa fedha za kutengenezewa barabara kwenye kata yake,alisema hiyo siyo kweli kwani bajeti ya ujenzi wa barabara inapagwa na madiwani wote.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.