|
Mashamba ya Kapunga na Mbarali sasa kuzalisha jetrofa badala ya mpunga
2008-05-11 11:51:22
Na Laurian Mkumbata, Mikumi
Wajumbe wa Bodi ya bonde la Rufiji, wamedai serikali ilitumia nguvu kubinafsisha mashamba ya umwagiliaji ya Kapunga na Mbarali kwa wawekezaji ambao hivi sasa wanakusudia kulima jetrofa badala ya mazao ya chakula.
Mwenyekiti wa bodi hiyo, Bw. Bakari Mbonde, alisema mashamba hayo yalipaswa kukabidhiwa kwa wananchi ili walime mpunga kwa ajili ya chakula.
Bw. Mbonde, alisema pamoja na kuishawishi serikali kuhusu manufaa ambayo yangepatikana kama wananchi wangepewa fursa ya umiliki wa mashamba hayo, ilikataa ombi hilo.
Alitoa kauli hiyo wiki iliyopita katika kikao cha Bodi kilichofanyika kwenye ukumbi wa VETA mjini hapa.
``Kabla ya kubinafsisha mashamba hayo kwa wawekezaji, tuliishauri serikali kwamba mashamba wapewe wananchi, jambo ambalo lingekuwa la manufaa zaidi kuliko wawekezaji, lakini wizara ilikuja juu na kusema serikali imeamua kuuza mashamba yake,``alisema.
Alisema kimsingi, wananchi walitakiwa kupewa kipaumbele cha kwanza katika umiliki wa mashamba hayo, na hata kiasi cha Sh bilioni tatu zilizopatikana katika uuzaji wake kwa wawekezaji hao, zingepatikana kutoka kwa wananchi.
``Kama suala lilikuwa ni kuboresha miundombinu, serikali ilikuwa na uwezo wa kuiboresha na wananchi wangerudisha gharama hizo kupitia ushirika wao, jambo ambalo lingekuwa na tija zaidi kuliko ilivyo sasa,``alisema.
Wawekezaji hao wanakusudia kulima jetrofa, zao linalotumika kuzalisha nishati ya kuendeshea mitambo, ingawa msingi wa uanzishwaji wa mashamba hayo ulikuwa kulima mazao ya chakula wakati wa kiangazi, ili kukabiliana na uhaba wa chakula nchini.
Naye Makamu Mwenyekiti wa bodi hiyo, Bw. Abed Mwasajone, alisema kuna haja ya kulitazama upya jambo hilo.
Alisema mradi wa kilimo cha umwagiliaji ulianzishwa katika eneo hilo kwa lengo la kulima mpunga kukidhi mahitaji ya chakula, hivyo hatua ya mwekezaji kulima jetrofa, inakiuka kusudi na malengo hayo.
Afisa Maji wa bonde la Rufiji, Bw. Willie Mwaluvanda, alikiri kupokea taarifa hizo kutoka kwa mwekezaji, kuhusu uamuzi wa kulima jetrofa badala ya mpunga.
Alisema ofisi yake haipo tayari kutoa kibali cha maji ya kumwagilia zao hilo, kwa vile maji hayo yanaruhusiwa kwa matumizi ya kilimo cha mpunga pekee.
Zoezi la kubinafsisha mashamba hayo lilileta mjadala miongoni mwa jamii, wakiwemo wanaharakati wa utetezi wa mazingira na haki za binadamu.
Jitihada hizo hazikuzaa matunda baada ya serikali kutamka kuwa mashamba hayo yalikuwa mali yake (serikali) hivyo wameamua kuyauza.
|