11 May 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Waaswa kuimarisha ulinzi wa miundombinu isiibiwe
 
2008-05-11 11:50:03
Na Mwandishi Wetu

Serikali imetoa wito kwa vikundi vya wananchi wanaomiliki miradi mbalimbali ya maji na ile ya kilimo cha umwagiliaji, kuhakikisha wanaimarisha ulinzi wa miundombinu yake ili kukabiliana na wizi wa vyuma chakavu.

Hayo yalisemwa jana na Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Bw. Christopher Chizza, wakati alipotembelea kisima cha maji katika kijiji cha Mivuleni, wilayani Moshi, ambacho maji yake yanavunwa kwa kutumia umeme wa jua (solar power).

Bw. Chizza alisema Wizara ya Maji imekuwa ikipata malalamiko mbali mbali kuhusiana na tatizo la wizi wa vyuma chakavu katika miundombinu ya maji na kushauri wasimamizi wa miradi hiyo kuanza kuchukua hatua za haraka kulinda wezi wa vyuma hivyo ili kukabiliana na tatizo hilo ambalo kwa kiwango kikubwa, linalozorotesha maendeleo katika sekta ya maji.

``Hakikisheni mnashirikiana ninyi kwa ninyi katika kukabiliana na wizi huu wa vyuma chakavu…wizi huu mbali ya kuharibu mifumo ya maji, pia imekuwa ikirudisha nyuma maendeleo yenu na ya serikali katika kujipatia maji safi na salama,`` alisema Chizza.

Akizungumzia mradi huo wenye uwezo wa kuzalisha kiasi cha lita 50 kwa sekunde moja, sawa na lita milioni mbili kwa siku, Bw. Chizza, aliwasisitiza wananchi kuendelea kulinda mradi huo na kulipongeza Kanisa la Kiinjili la Kilutheri nchini (KKKT) kwa ufadhili wa mradi huo.

Mradi huo wenye visima viwili vilivyochimbwa mwaka 1992 chini ya shirika la OXFAM, umewekewa pampu inayoendeshwa kwa umeme wa jua, wenye gharama ya Sh. milioni 56 ambapo maji yake hutumiwa kwa ajili ya kilimo pamoja na shughuli nyingine za kijamii.

Aliwataka wakazi wa kijiji hicho na vijiji vya jirani wanaonufaika na mradi huo kuhakikisha wanautunza kwa nguvu zao zote ili hatimaye uweze kuwa mkombozi wao na familia zao.

Alisisitiza umuhimu wa wananchi kuthamini kitu chao na kuacha tabia ya kuharibu miundombinu kwa kuuza vyuma chakavu ili kujipatia fedha kidogo hali aliyoisema kuwa itawaletea matatizo makubwa pamoja na ukosefu wa maji.

``Msikimbilie kung`oa vyuma kwa ajili ya kupata ujira mdogo, wafadhili walituamini, ndio maana walituletea neema hii ya maji, zingatieni na itumieni na kuilinda kama mlindavyo mboni za macho yenu…serikali iko nanyi katika kila jambo kama ilivyo katika ilani ya chama cha mapinduzi,`` alisisitiza.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.