|
Mbunge alilaumu jeshi la Polisi kushindwa kudhibiti uhalifu
2008-05-11 11:49:15
Na Simon Mhina
Mbunge wa Tarime Bw. Chacha Wangwe (CHEDAMA) amesema mapigano ya kikabila na Koo yanayozuka kila mara katika jimbo hilo, yanachochewa na Sungusungu kwa maslahi ya kisiasa.
Aidha Bw. Wangwe amelilaumu Jeshi la Polisi kwa kushindwa kudhibiti matukio ya ujambazi hatua inayowafanya wananchi waishi kwa wasiwasi.
Akizungumza na Nipashe jijini Dar es Salaam, Bw. Wangwe alisema licha ya kwamba jeshi la Sungusungu halipo kwa mujibu wa katiba ya nchi, lakini `askari` wanatokana na wanachama wa jumuiya ya vijana wa chama tawala UVCCM.
Alisema hakuna mpinzani yeyote ambaye ni sungusungu.
Alisema kutoakana na kutokuwa na mafunzo ya ulinzi, sungusungu hao wamekuwa wakitumia ubabe na kuchochea vurugu katika jamii.
``Ukisikia koo fulani zinapigana Tarime, ujue wanaopigana ni sungusungu kwa maslahi ya kisiasa, hakuna watu wanaopenda kupigana kule,``alisema.
Alisema ndio maana licha ya sungusungu kuwepo kila kijiji, ujambazi unashamiri, kwa vile kazi yao hutumika kisiasa zaidi kwa kuwanyanyasa wananchi.
Bw. Wangwe ambaye pia ni Makamu mwenyekiti wa CHADEMA alisema miezi miwili iliyopita, kumekuwa na matukio ya ujambazi ambayo yanafumbiwa macho na polisi.
Alisema wakati polisi wanadai kuwa hawana uwezo, juzi wamepelekwa askari zaidi ya 1,000 pamoja na helkopta iliyosheheni silaha nzito, kwa ajili ya kwenda wakudhibiti wananchi waliodaiwa kuvamia mgodi wa North Mara unaomilikiwa na kampuni ya Barrick.
``Askari elfu wanatumika kumlinda mwekezaji lakini wananchi wakivamiwa na majambazi, wanaambiwa hakuna Polisi,``alilalamika.
Alisema ni juzi majambazi yalivamia Kijiji na Kitenga Kata ya Bumera jimboni hapo na kuumiza wananchi na kuwapora.
Bw. Wangwe alisema Chadema kimegundua kuwa polisi wanafumbia matukio hayo kwa makusudi kwa maelekezo ya CCM, ili wawezekutumia agenda hiyo kwenye uchaguzi mkuu ujao.
Aliwataka wananchi wa jimbo la Tarime lenye Kata 20 kutolitegemea tena jeshi la polisi katika kujihami, kwa vile limepewa maelekezo ya kuwatelekeza, badala yake wajilinde wenyewe.
Mbunge huyo alisema matukio ya ujambazi, mapigano ya koo, ni vita ya kisiasa dhidi ya Chama chake.
Bw. Wangwe alisema chakushangaza matukio hayo yanaambatana na kuumizwa na kuporwa kwa viongozi wa kisiasa waliochaguliwa kwa tiketi ya Chadema.
Mbunge huyo alilalamikia vitendo vya viongozi hao kubambikiwa kesi na kuswekwa rumande.
Alisema majuzi makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya Tarime,ambaye anatokana na Chadema, Bw. Tengera Marwa amebambikiziwa kesi na hadi sasa yupo ndani.
|