|
Bajeti ya Serikali isiwe tegemezi kwa misaada ya wahisani
2008-05-11 11:48:02
Na Mhariri
Jumuia ya Ulaya (EU) hivi karibuni ilifanya uamuzi wa kukubali kuendelea kuisaidia Tanzania katika bajeti na miradi mingineyo ya maendeleo, hali hiyo ni ya kupongezwa ikizingatiwa kuwa inaipa uwezo serikali ya kutoa huduma bora zaidi kwa maendeleo ya wananchi wake.
Uamuzi wa Jumuia ya Ulaya kukubali kufadhili sehemu ya bajeti ya Serikali ni ushahidi dhahiri kuwa ina imani na matumizi ya fedha hizo kuwa zinalenga katika makusudio yaliyotarajiwa ambayo ni kusaidia maendeleo katika nchi, na yanatafsiri maendeleo ya maisha ya wananchi wa kawaida.
Tanzania ina vyanzo vingi vya mapato ambavyo kama vingedhibitiwa kwa ukamilifu, mapato hayo yangeweza kupunguza hali yanchi kiuchumi kutegemea wahisani na misaada mingine toka nje.
Ni jambo lisilofichika kuwa nchi hii ina utajiri wa asili unaotokana na madini, utalii, uvuvi na kilimo cha mazao ya biashara.
Mkazo katika usimamizi na udhibiti wa mapato yatokanayo na maeneo hayo unaweza kupunguza kwa kiwango kikubwa kwa Serikali kuendelea kutegemea misaada na ufadhili kutoka nchi wahisani wakati wa kupanga matumizi ya fedha katika wizara.
Ni dhahiri pia kuwa amani na utulivu uliopo nchini umechangia kwa kiwango kikubwa kuvutia wawekezaji ambao miradi yao mbalimbali wanayowekeza hapa nchini inalipatia Taifa fedha za kutosha kutokana na kodi zinazolipwa pamoja na malipo mengine.
Jambo la msingi ni udhibiti na usimamizi wa mikataba ya hao wawekezaji hasa wale wanaowekeza katika sekta za madini na uvuvi ambako usimamizi wake unahitaji umakini kutoka kwa wataalamu wa idara hizo.
Kwa kutambua kuwa kuna wakati uhisani na misaada kutoka kwa wafadhili unaweza ukakoma, serikali inatakiwa iweke mikakati mbadala ya kuweza kujikusanyia mapato ili hatimaye iweze kujitegemea katika bajeti yake, hali hiyo itaweza kupunguza kwa kiwango kikubwa kwa bajeti kuwa tegemezi.
Imefahamika kuwa katika bajeti ya mwaka huu, serikali inategemea asilimia arobaini na moja ya bajeti hiyo kutoka kwa wahisani, na kwamba mwaka ujao itakuwa asilimia arobaini, kasi hiyo bado haitii moyo ikilinganishwa na uwezo asili uliopo nchini.
Yapo matatizo ambayo yanaweza kuwa ni kikwazo katika kufanikisha azma ya serikali ya kupunguza utegemezi wa bajeti toka kwa wahisani, moja ya matatizo ni majanga ya ukame, ufisadi na hujuma nyingine za kiuchumi.
Mwakilishi wa EU katika Tanzania Balozi Clarke, alieleza hivi karibuni kuwa wao wameridhishwa na hatua zinazochukuliwa na serikali ya Tanzania katika kupambana na maovu kama ufisadi na uwazi wa serikali katika matumizi ya fedha za wahisani ambazo alisema zinalenga katika kuleta maendeleo ya wananchi.
Katika kipindi hiki ambacho kumekuwa na tuhuma mbalimbali za kuhujumu fedha za serikali, ambapo wahusika wakuu ni baadhi ya viongozi waliokuwa serikalini, na ambao wengine tayari wameshajiuzulu, upo umuhimu mkubwa wa kuwa waadilifu wa hali ya juu katika kusimamia fedha za umma, ili maisha ya wananchi yabadilike na kuwa yenye neema zaidi.
|