11 May 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Bwana mzee amjengea nyumba bi-mdogo lakini bi-mkubwa akaiwahi
 
2008-05-11 11:46:56
Na Anti Flora Wingia

Mpenzi msomaji, kitimtim kuhusu vimbwanga vya nyumba ndogo bado sijavimaliza. Wiki iliyopita utakumbuka nilidodosa pale nyumba ndogo inapogeuka kuwa nyumba kubwa huku ile nyumba kubwa ikiachwa solemba.

Leo hebu nikumegee kituko kingine ambapo nyumba kubwa imeipiku nyumba ndogo ambayo ilijaribu kuhamia kwenye nyumba mpya iliyojengwa na bwana mzee bila mafanikio. Ilikuwaje? Vuta subira.

Unajua mpenzi msomaji hizi nyumba ndogo pamoja na wazee wengine kuzithamini na kuziegemea, lakini zina mitafaruku kibao.

Wenyewe wanaziita sabuni za roho, mara kipima joto na wengine huziita viboresha maisha na kadhalika. Lakini wakati mwingine utamu wa nyumba hizi hugeuka shubiri.

Yupo baba mmoja niliyesimuliwa kituko chake majuzi aliyekuwa na familia yake nzuri na aliyefanya kazi serikalini kwa muda mrefu hadi kustaafu.

Mkewe hali kadhalika alikuwa mwajiriwa katika kiwanda fulani ambako pia alistaafu miaka kadhaa iliyopita.

Huku wastaafu hawa wakiwa bado wanaishi pamoja katika nyumba ya kupanga, baada ya kuwa na watoto kadhaa, watoto wale nao wakaolewa na kuoa hivyo sasa kuwa na wajukuu.

Ndugu za baba huyu ambao wana nyadhifa serikalini wakamtafutia eneo kubwa la shamba ili aweze kuendeleza maisha na familia yake. Shamba lile akaliendeleza ambapo pia alijenga nyumba yake nzuri ya kuishi.

Kilichotokea ni kwamba wakati baba huyu akipatiwa shamba lile na kuanza ujenzi, watoto wake ambao wengine wameolewa, walipata taarifa.

Hivyo wakawa na furaha kuwa angalau sasa mama yao(bi-mkubwa) atakuwa na maskani ya kudumu na kuondokana na kero za upangaji.

Wakati watoto wakidhani hivyo, kumbe baba yao alikuwa na nyumba ndogo aliyoithamini kuliko kitu kingine chochote. Tangu anapewa shamba lile na kuanza ujenzi hadi unamalizika alikuwa akiwa sambamba na bi-mdogo.

Inavyoonekana, baba huyu hakujua kama watoto wake wakubwa wanafahamu juu ya ujenzi ule.

Kisanga kilianza pale watoto hawa walipojulishwa na jamaa yao fulani kuwa nyumba ilishamalizika na wasipofanya haraka kuhamia watakijikuta wakizidiwa kete na nyumba ndogo ambayo tayari walishajua ipo.

Watoto wale wakajiandaa wakamchukua mama yao na kujitosa kwenye nyumba yao mpya iliyoko nje kidogo na jiji la Dar es Salaam. Baada ya hatua hiyo, ndipo watoto wale wakamwendea baba yao na kumwambia walichokifanya na kwamba yeye naye akaungane nao huko makazi mapya, hivyo kuachana na nyumba za kupanga mjini.

Habari zinasema kuwa baba yule kwanza hakuamini walichoamua watoto wake kwani alitegemea kwenda kuishi katika makazi yale mapya na bi-mdogo.

Ingawa alipata kizunguzungu cha muda, lakini baadaye ilibidi akubali hali halisi na kwenda kuungana na familia yake.

Swali linakuja, je, bi-mdogo yule alijisikiaje baada ya kuona nyumba aliyosimamia ujenzi wake hadi kuisha, lakini hakuweza kuishi mle baada ya watoto kumzidi kete baba yao na kumtanguliza mama mzazi?

Mpenzi msomaji, hizo ndizo dhoruba zinazojitokeza pale nyumba ndogo na kubwa zinapojikuta ulingoni. Bwana mzee anamjengea nyumba bi-mdogo, lakini fumba na kufumbua bi-mkubwa anajitosa na kuhamia.

Mambo hayo, au siyo? Ah! Maisha Ndivyo Yalivyo.
Bado nalia na kinababa wanaoishusha hadhi nyumba kubwa ambayo naamini ndiyo iliyomfikisha hapo alipo na badala yake kuithamini nyumba ndogo ambayo wakati mwingine hukaa tu mezani na kula vilivyoandaliwa.

Lakini sijui hulka za wanadamu wengine zikoje. Utakuta mke ndiye aliyemleta mumewe mjini, akamuonyesha mitaa na hata kufanikiwa kupata kazi. Watazaa watoto na katika mihangaiko wakafanikiwa kupata watoto kadhaa, na kuwasomesha.

Pamoja na mwanzo mgumu, hatimaye kubahatika kupata mafanikio makubwa, baba huyu anasahau yote yale na kuanza kumnyanyasa mkewe, kisa eti katika pepesa pepesa macho kaona vimwana warembo na wabichi wenye uwezo wa kumliwaza kuliko mkewe ambaye sasa ni mtu mzima(mzee).

Siyo siri, wapo kinababa ambao hawaamini kwamba umri umeshapita na hivyo wanapaswa kufanya mambo yenye hekima na yasiyofedhehesha.

Lakini hawa ndio utakuta wanawarubuni watoto wetu wanafunzi au kuiba kwa usiri wake za watu huku nyumbani wakiwa na wake zao watulivu na wenye uwezo katika huduma zote za kifamilia.

Lakini niwaambie hawa wazee wapenda dogodogo ambapo pia wapo kinamama (mashugamami) wenye kijitabia hicho, kwamba mahusiano ya pembezoni ni hatari na yenye kuvuruga maisha ndani ya familia zetu.

Hakuna familia iliyo imara ambayo pembeni mwake imejichimbia nyumba ndogo.

Kila wakati ni mitafaruku huku nyingine zikivunjika, wengine wakifukuzana kama chui na swala, kisa chungu kipya kimepatikana, hivyo kile cha zamani kinapigwa mateke.

Watoto niliozungumzia mwanzoni mwa makala hii walichukua uamuzi wa busara sana. Hawakuona sababu mama yao kufanywa second-hand na kubakishwa nyumba za kupanga huku baba yao akisuuza nafsi yake na bi-mdogo katika nyumba mpya.

Huo ni ujumbe tosha kwa wazee wenye tabia ya kupuuza nyumba zao kubwa na kuegemea nyumba ndogo.

Kama wapo watoto sasa wamefumbua macho na katu hawakubali kuona mama yao ananyanyaswa huku wakitazama.

Ujasiri huu ni mzuri yafaa kuigwa. Nyumba kubwa ndizo msingi wa maisha ndani ya familia zetu, hizi ndogo ni walaji tu na si watafutaji.

Masomaji wangu kwa leo niishie hapa, kama unayo maoni au kituko chochote kuhusu maisha yetu ya kila siku usisite kunikandamizia kupitia email ifuatayo:-
fwingia@yahoo.com
Wasalaam.

  • SOURCE: Nipashe
Tuma Maoni Yako
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.