|
Basi laua 12 Moro
2008-05-10 11:42:12
Na Fitina Haule, PST, Morogoro
Watu 12 wamefariki dunia na wengine 29 kujeruhiwa vibaya baada ya basi la Kampuni ya Alhooshom kuparamia tela la lori katika eneo la Msimbai kijiji cha Kiegea, wilayani Kilosa mkoani Morogoro.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, Bw. Thobias Andengenye alisema tukio hilo lilitokea jana, saa 3:45 katika eneo hilo.
Alisema ajali hiyo ilihusisha magari yenye namba T365AAK aina Scania lililokuwa likitokea Morogoro kwenda Dodoma, likiendeshwa na Thomas Magosho na kugongana na lori lenye namba T188AGF lililokuwa na trela lenye namba T230ACR aina ya Scania lililokuwa likitokea Dodoma kwenda Dar es Salaam likiwa limebeba mahindi.
Kamanda Andengenye alisema basi hilo liligonga trela la Scania baada ya trela hilo kukatika kutoka kwenye kichwa chake na kukatisha barabara na ndipo basi hilo lilipojigonga kwenye trela na kusababisha ajali hiyo.
Alisema katika ajali hiyo watu waliokufa ni wanaume wanane akiwemo dereva wa basi hilo na kondakta wake na wanawake wanne.
Kwa mujibu wa Bw. Andengenye, maiti watano wametambuliwa kati ya 12 na ndugu zao wamejaza fomu za kuwachukua.
Bw. Andengenye aliongeza kuwa katika ajali hiyo kuna majeruhi 29, ambapo kati ya hao 20 wamelazwa katika hospitali ya Berega na tisa wamepelekwa hospitali ya mkoa wa Morogoro kutokana na hali zao kuwa mbaya.
Akizungumzia ajali hiyo, Daktari wa Hospitali ya Wilaya ya Kilosa, Dk. John Lindi, alisema watu waliofariki wote walifia eneo la ajali na kwamba hakuna aliyefia hospitalini hapo.
Dk. Lindi aliwataja majeruhi wa ajali hiyo kuwa ni Saren Robert, Nasibu Mlunge, Malingumu Leguna, Wiston Amos, Ramadhan Ally, Ally Athumani, Ujari Jumanne, Shaban Kikoti, Wema Maja, Msofe Wilson, Jeswad Mawanja, Athuman Mohammed, Jumanne Idd, Mshombe Mputa, Nissan Hoiya na Kindamali Kicheroda.
Wengine ni Francis Chilongola, Abdulrashid Kindamba, Ernest Mnyandwa, Grace Flavian, Esta Sebanga, Jane William, Baraka Isaya, Debora Msanya, Kevin Chilongola, Mwajuma Kusupa, Rehema Halune, Melania Masota na Pascalina Shamte.
Naye mmoja wa majeruhi wa ajali hiyo, Bw. Malingumu Leguna (20), mkazi wa Gairo alisema ajali hiyo ilitokea wakati lori aina ya Scania lilipokuwa likilipita gari jingine lililokuwa mbele yake na kukutana na basi walilokuwemo.
Alisema baada ya dereva wa lori hilo kuliona basi lao alijaribu kurudi upande wake hali ambayo ilisababisha trela la lori hilo kukatika kutoka kwenye kichwa chake na kuziba barabara.
Alisema baada trela hilo kuziba barabara na kutokana na mwendo kasi aliokuwa nao dereva wa basi lao, alishindwa kushika breki na kujikuta akiligonga trela hilo na kusababisha ajali hiyo.
Dereva wa lori aina ya Scania lililosababisha ajali hiyo amekimbia na polisi wanaendelea kumsaka.
|