|
Bunge kupitia sheria ya maadili
2008-05-10 11:41:13
Na Mashaka Mgeta
Spika wa Bunge, Bw. Samuel Sitta, ameagiza kupitiwa upya kwa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, ili kubaini mapungufu yanayohitaji kufanyiwa marekebisho.
Bw. Sitta ambaye pia ni Mbunge wa Urambo Mashariki (CCM) mkoani Tabora, alitoa agizo hilo, wakati akiwa katika ziara ya kikazi jimboni humo na chombo chenye jukumu la kupitia sheria hiyo Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala.
Hata hivyo, Sheria hiyo namba 13 ya mwaka 1995, imepingwa na asasi kadhaa ya kijamii, kupitia kesi iliyofunguliwa katika Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam.
Asasi hizo zinadai kuwa, pamoja na athari nyingine, ibara za 6(1), (2) na 7(2) (c) za sheria hiyo, zinazuia wananchi kupata taarifa zinazotolewa na viongozi wa umma kuhusu rasilimali, mapato na madeni yao.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam jana, Katibu wa Spika, Bw. Daniel Eliufoo, alisema uamuzi huo unakidhi matakwa ya kulifanya Bunge kuwa katika nafasi nzuri ya kupata majawabu ya matatizo, migogoro na kero zinazowakabili wananchi.
Bw. Eliufoo, ambaye hakutaka kutoa ufafanuzi wa kina, kwa madai kuwa mwenye mamlaka hayo ni Bw. Sitta, alisema agizo hilo limetolewa na Spika kwa njia ya maandishi, kwenda kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ya Bunge, Bw. George Lubeleje.
Alisema kupitiwa kwa sheria hiyo ni miongoni mwa hatua zitakazochukuliwa na Spika kuwasilisha kwa Kamati za Bunge, masuala mbalimbali yanayolalamikiwa na jamii, wadau na umma kwa ujumla.
Kwa mujibu wa Bw. Eliufoo, uamuzi huo unakubalika kutokana na kanuni ya 116 ya kanuni za Bunge, toleo la 2007 inayosema, ``Spika aweza kukabidhi jambo lolote kwa kamati yoyote kadri atakavyoona inafaa, kwa ajili ya kushughulikiwa na kamati hiyo.``
``Kwa kuanzia, Spika ameagiza kuwa katika kipindi kijacho cha vikao vya Kamati za Bunge hapa Dar es Salaam, Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala itapitia sheria ya maadili ya viongozi wa umma namba 13 ya mwaka 2007, ili kubaini mapungufu yanayolalamikiwa na wananchi kwa muda mrefu sasa,`` alisema Bw. Eliufoo.
Vikao vya Kamati za Bunge, vitaanza jijini Dar es Salaam Mei 26, mwaka huu, ambapo pamoja na mambo mengine, kamati hizo, zitapitia rasimu ya bajeti itakayosomwa bungeni katika mkutano utakaoanza mwezi ujao.
``Hii ni mojawapo ya kazi zitakazoshughulikiwa na kamati hiyo kwa kipindi ambacho Kamati za Bunge zitakuwa zinaendelea na vikao vyake,`` aliongeza.
Bw. Eliufoo, alisema baada ya kuipitia na kuitafakari sheria hiyo kwa kina, kamati husika itatoa mapendekezo yatakayowasilishwa bungeni na hatimaye serikalini kwa hatua zaidi.
``Msingi wa hatua hii ni kuziwezesha Kamati za Bunge kuwa `proactive` kwa kulisaidia Bunge kutafuta majawabu ya matatizo, migogoro na kero mbalimbali zinazowakabili wananchi na jamii kwa ujumla,`` alisema.
Aidha, Bw. Eliufoo alisema uamuzi huo wa Spika, utaliwezesha na kuliweka Bunge katika nafasi nzuri zaidi ya kutekeleza kwa ufanisi majukumu yake ya kikatiba, yanayoanishwa kwenye ibara ya 63(2).
Malalamiko dhidi ya sheria hiyo yaliibuka baada wananchi mbalimbali, waandishi wa habari, wanaharakati na viongozi wa vyama vya siasa kutinga katika ofisi za Tume ya Maadili jijini Dar es Salaam ili kujua mali za baadhi ya viongozi wanaotuhumiwa kwa kujilimbikizia mali.
Wananchi hao walitaka kujua mali walizoorodhesha viongozi hao, na zile wanazodaiwa kuwa nazo.
Kwa viongozi wastaafu, wananchi walitaka kujua mali walizoorodhesha katika Tume hiyo wakati wakiingia madarakani na zile ambazo walizitaja wakati wakiacha madaraka.
Baadhi ya viongozi ambao wananchi walitaka kujua mali zao zilizoorodheshwa ni Bw. Andrew Chenge, Rais Mstaafu Benjamin Mkapa na aliyewahi kuwa Waziri wa Fedha katika serikali ya Awamu ya Tatu, Basil Pesambili Mramba.
Hata hivyo, walikumbana na sheria hiyo inayokataza mtu kutangaza mali za kiongozi yeyote kwa mtu mwingine, hata kama ataruhusiwa `kuperuzi` faili lenye orodha ya mali zake baada ya kuomba.
|