|
Petroli, dizeli vyasababisha mfumuko wa bei Pemba
2008-05-10 11:39:41
Na Mwinyi Sadallah
Kisiwa cha Pemba, kimekumbwa na mfumuko mkubwa wa bei za mafuta ya dizeli na petroli na kusababisha sekta ya usafirishaji kuathirika.
Mfumuko huo wa bei umeanza kujitokeza wiki hii baada ya viwango vipya vya bei kuanza kutumika katika vituo mbalimbali vya usambazaji mafuta kisiwani humo.
Mafuta ya dizeli kisiwani humo sasa yamepanda bei kutoka Sh. 1,480 hadi Sh. 1,825, wakati petroli imepanda kutoka Sh. 1,490 hadi Sh.1,615.
Kwa mujibu wa barua ya Mkuu wa Idara ya Nishati Zanzibar ya Mei 7, mwaka huu, Bw. Omar Juma Khamis, imemtaka Ofisa Mdhamini wa Wizara ya Maji, Ujenzi, Nishati kisiwani humo, kusimamia viwango vipya vya bei katika vituo vyote vya soko la jumla katika maeneo ya Wesha.
Viwango vya bei vilivyopangwa katika soko la jumla ni dizeli lita Sh. 1,795, petroli Sh. 1,585 na mafuta ya taa Sh. 1,430.
Kutokana na mabadiliko hayo, hivi sasa mafuta ya taa kisiwani Pemba yamepanda bei kutoka Sh. 1,060 hadi Sh. 1,460.
Uchunguzi wa Nipashe umebaini kwamba, hali hiyo imesababisha sekta ya usafirishaji kuathirika kutokana na bei za nauli kuongezeka ambapo magari ya abiria yanalazimika kupandisha bei jambo linalozua malalamiko mengi kutoka kwa wananchi.
Abiria wanaosafiri kutoka mkoani hadi Chake Chake wanalazimika kulipa Sh. 1,500 badala ya Sh. 1000 pamoja na miji wa Chake Chake - Wete, wakati kutoka Chake Chake hadi Konde wanalipa Sh. 2,000.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi walisema wanashangazwa na kiwango hicho cha bei ya mafuta kutofautiana na viwango vya bei vinavyotumika kisiwani Unguja.
Bw. Hamad Kombo, mkazi wa Wete alisema kwamba hivi karibuni mafuta yalipandishwa bei kisiwani Unguja, ambapo petroli inauzwa Sh. 1,660, badala ya Sh. 1,490, wakati dizeli inauzwa kati ya Sh. 1,560 hadi Sh. 1,580 kwa lita kutoka Sh. 1,350.
``Kwa kweli viwango hivi vya bei vimeanza kutuathiri sisi wananchi kwa vile kila unapokwenda bei ya nauli imepanda,`` alisema Bw. Kombo.
Tangu mafuta kupanda katika soko la dunia kutoka pipa moja dola za Merekani 110 hadi 116 kumekuwepo na wimbi kubwa la kupanda bei ya bidhaa hiyo katika miji ya Unguja na Pemba na kusababisha mfumuko wa bei za vyakula hasa vijijini.
Kampuni zinazoingiza mafuta kisiwani Pemba kampuni ya Zanzibar Petroleum (ZP) pamoja na ile ya GAPCO, lakini wasemaji wa kampuni hizo hawakuweza kupatikana kueleza tafauti hizo kati ya Unguja na Pemba.
|