|
Ukarabati Uwanja wa Taifa na Karume uchuguzwe
2008-05-10 11:19:43
Na Mhariri
Uwanja wa zamani wa Taifa umefanyiwa ukarabati mkubwa na kuwekwa nyasi bandia ili kuuboresha zaidi na kuufanya uwe wakisasa.
Uwanja huo unaomilikiwa na Serikali, mbali na kutumika kwa shughuli mbalimbali za kitaifa kama hafla za Uhuru, Muungano au hata kuapishwa kwa marais wanaochaguliwa kuongoza Tanzania, sasa umekuwa kero kubwa kutokana na kusimamisha maji katikati na hivyo kufanya baadhi ya mechi kuahirishwa au zingine kufutwa kabisa.
Pamoja na fedha nyingi kutumika kuukarabati uwanja huo, lakini matatizo ya kujaa maji yamekuwa kero kubwa kwa wachezaji na hata wakati mwingine kwa wapenzi pale mechi zinapolazimika kuahirishwa.
Hivi karibuni timu yetu ya taifa, Taifa Stars, ilitarajiwa kucheza mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Msumbiji ambayo ilijitahidi kuwaita karibu nyota wake wote wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi, lakini mchezo huo ulishindwa kufanyika baada ya mvua kunyesha na kujaza maji uwanjani.
Mchezo huo ulishindwa kufanyika siku nyingine tena kwani wachezaji wa kulipwa wanaosakata kabumbumbu nje ya nchi wamekuwa wakipewa ruhusa maalum na wanatakiwa warejee katika timu zao kwa wakati uliopangwa na sio kuzubaa zubaa na ndio maana walishindwa kucheza mechi siku nyingine, licha ya TFF, Shirikisho la Soka Tanzania, kubembeleza mchezo huo ufanyike siku nyingine.
Na sio mchezo huo tu, pia ule wa Stars na Harambee Stars ya Kenya ulichelewa kuanza kwa kuwa mvua ilinyesha na kusababisha maji kujaa uwanjani.
Mbali na mifano hiyo michache pia mechi kadhaa za Ligi Kuu Tanzania Bara zimewahi kuahirishwa sababu za maji kujaa uwanjani na kushindwa kufanyika kutokana na ufinyu wa miundo mbinu ya kutoa maji.
Hali kama hii haliwezi kuendelea kuvumiliwa kwani wahusika wa uwanja huo wanatakiwa waeleze bayana kuwa nini kilikosewa hadi kusababisha uwanja kuwa unajaa maji wakati wa mvua licha ya FIFA, Shirikisho la Kimataifa la Soka, kutoa fungu kwa ajili ya ukarabati.
Ni haki yao wananchi kujua hilo kwani uwanja huo ni wao na kama FIFA walibabaisha katika kutoa fedha na hilo liwekwe bayana bila kificho au kama shirikisho hilo lilitoa fedha kiduchu, basi na hilo nalo liwekwe bayana.
Hata hivyo, inawezekana kuna hujuma za kifisadi zilifanyika, hivyo, wakati umefika sasa kwa Serikali kuchunguza hata vyombo vya michezo ambavyo vimekuwa vikilalamikiwa kwa kipindi kirefu kwa ufisadi, ili wahusika wafikishwe katika vyombo vya sheria.
Mara nyingi vyombo vya michezo vimekuwa vikisahaulika na kuwafanya baadhi ya watu hasa wale viongozi wake kujiona kama wanaweza kufanya watakacho bila ya kuingiliwa au kuulizwa na mtu hata kama watakula michango au ada za wananchi.
Kwa kweli katika michezo kuna uozo mwingi, ambapo yapo madai ya kiongozi au viongozi kula pesa lakini hakuna wa kuwauliza, si nani wala BMT, Baraza la Michezo la Taifa, lenye dhamana ya michezo nchini.
Wakati umefika kwa mafisadi wote katika michezo kushughulikiwa kwani wamekuwa wakijiona kama vyama au taasisi wanazoziongoza ni zao, wakati wamepewa dhamana ya kuviongoza tu katika harakati za kuleta maendeleo katika michezo nchini.
Mbali na Uwanja wa Taifa, ambao hutumika kwa mechi mbalimbali za kitaifa na kimataifa, pia uwanja wa Karume ambao timu zetu za taifa zinautumia, nao pia una kasoro kibao licha ya uwanja huo pia kufanyiwa ukarabati na FIFA hiyo hiyo.
Timu yetu ya taifa inatakiwa kuwa na sehemu nzuri ya kufanyia mazoezi ili iweze kujiandaa vizuri kwa ajili ya kuwa tayari kwa mashindano mbalimbali ya kimataifa.
Tunaomba ukarabati wa Uwanja wa Taifa na ule wa Karume uchuguzwe na wahusika wahojiwe ili kujua nini hasa kinachosababisha viwanja hivyo kuwa katika hali duni, hasa inaponyesha mvua, licha ya kufanyiwa ukarabati mkubwa.
|