10 May 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Taifa Cup halina vipaji?
 
2008-05-10 11:18:27
Na Daniel Mkate

Hivi sasa jiji la Dar es Salaam, limeingiliwa na wageni mbalimbali toka mikoa 20 kwa ajili ya kushuhudia michuano ya kombe la taifa.

Jumla ya mikoa 23 toka Tanzania Bara inashiriki michuano hiyo ya mtoano, huku mkoa wa Dar ukiwa na `mikoa` mitatu ndani yake.

Mikoa hiyo ni Kinondoni, Ilala na Temeke, ambayo imepewa hadhi ya mikoa kutokana na wingi wa wachezaji wake ndani ya Jiji la Dar es Salaam.

Pamoja na nia nzuri ya Shirikisho la Soka nchini (TFF), kufufua michuano hiyo kwa msimu wa tatu sasa, lakini naamini kuna mapungufu makubwa ndani yake tofauti na malengo ya michuano yenyewe.

Michuano hiyo ambayo imekusanya wachezaji 460 toka mikoa yote 23, ilitegemea kutoa wachezaji wengi wenye vipaji kutokana na kuonyesha uwezo wao wa kiuchezaji uwanjani.

Lakini kutokana na hali ya uendeshaji wa michuano hiyo hivi sasa, ni vigumu mno kufikia kupata vipaji vya wachezaji walengwa katika michuano yenyewe.

Lengo la TFF kusaka wachezaji wenye vipaji toka mikoa yote nchini, inawezekana ni ndoto zisizo na usingizi, kwani mfumo wa uendeshaji wake ni vigumu kugundua kipaji cha mtu.

Kwa akili timamu, timu iliyojiandaa kwa kipindi kirefu na kuweka maandalizi ya mazuri ya ushiriki kwa ajili ya mkoa kutoa wachezaji wenye vipaji, inakuwa ni hatari pale inapoingia uwanjani kwa mechi moja na kutolewa.

Kwa kila mkoa kusajili wachezaji 20, halafu wakatumia 15 kwa mchezo mmoja unamalizika kwa timu kufungwa huku `vifaa` vingine vikiwa nje, haiwezekani kabisa kufahamu ni mchezaji yupi anafaa kwa kipaji.

Kwa mfano, timu zetu za Simba na Yanga, zimewahi kukimbilia kusajili wachezaji `wabovu` kwa gharama kubwa, kutokana na tu mchezaji huyo kuonyesha kiwango kizuri katika mechi moja.

Hivyo, basi kwa mchezaji wa namna hiyo, ilitakiwa aangaliwe zaidi ya mechi mbili ndipo apimwe uwezo wa kipaji chake na wala si kuangaliwa kwa siku moja.

Aidha, michuano ambayo kwa kipindi kirefu imekuwa ikiendeshwa bila udhamini, kwa sasa inadhaminiwa na Safari Lager.

Lakini, kwa muonekano wa michuano yenyewe, wadhamini ndio wameonekana wenye nafasi kubwa zaidi kuliko wasimamizi wa michuano hiyo, TFF, ambao awali walikuwa na lengo zuri la kusaka vipaji.

Ama labda kwa kutambua wingi wa timu au gharama kubwa za timu shiriki, michuano hiyo inashindanishwa kwa hatua ya mtoano ili kuweza labda kutangazwa kinywaji cha wadhamini.

Pamoja na hayo, ili kusaka vipaji vya wachezaji, TFF ilitakiwa kutoruhusu ama kuruhusu wachezaji wasiopungua watano tu wa Ligi Kuu kwa mkoa mmoja, ili kuwapa nafasi chipukizi.

Kuwapa nafasi wachezaji chipukizi, ni kutafuta vipaji vinavyotakikana, lakini kwa mtindo unaotumika sasa katika michuano inayoendelea ndani ya uwanja wa zamani wa Taifa, ni kufurahishana tu kati ya TFF na wadhamini.

Kushirikisha lundo la wachezaji wanaoonekana katika michuano ya Ligi Kuu na kuwaacha chipukizi wenye vipaji, kunahatarisha kudororesha michuano hiyo ya kitaifa.

Inawezekana, kukosekana kwa muda ndiko kunasababisha michuano hiyo kuendeshwa kwa mtoano, lakini ni kitu cha kujiuliza zaidi na zaidi.

Mwaka jana na mwaka juzi, michuano hiyo ilikuwa haina wadhamini, lakini iliendeshwa kwa timu kucheza mechi mbili mbili za nyumbani na ugenini, iweje kipindi hiki michuano yenye udhamini ikaendeshwa namna hiyo.

Yote tuache, lakini kuna uwezekano mdogo kuweza kupata vipaji katika michuano hii na matokeo yake kumpa lawama kocha mkuu wa timu ya taifa, Taifa Stars, Marcio Maximo, kuwa ameshindwa kuteua wachezaji kwenye Kombe la Taifa.

Naombea tupate wachezaji wenye vipaji na si bora vipaji. Tuzingatie vipaji vinapatikanaje, na wala si kukimbilia ili mradi wadhamini wametaka iwe kama wanavyotaka.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.