10 May 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Sportsnews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Simba: Yanga ruksa kumchukua Yondani
 
2008-05-10 10:30:19
By Badru Kimwaga

Uongozi wa klabu ya soka ya Simba umesema kuwa hauna tatizo kwa watani zao Yanga kumsajili beki wao Kelvin Yondani `Materazzi`, ilimradi wafuate na kuzingatia taratibu za usajili zilizopo ikiwemo kufanya mazungumzo nao juu kuwaachia wamchukie akawatumikie.

Aidha, uongozi huo wa Simba hauna mpango wowote wa kumsajili mchezaji yeyote toka Yanga kwa madai kwamba hawana viwango wala uwezo wa kuichezea timu yao.

Mhazini Msaidizi wa klabu hiyo, Chano Almasi, alisema jana jijini kuwa, uongozi wao hauna kikwazo kwa Yanga kumsajili Kelvin Yondani iwapo wamerisdhishwa na kiwango chake, ilimradi wafuate taratibu.

Chano alisema kuwa, sio kwa Yondani tu, bali mchezaji yeyote anayetakiwa na Yanga ama timu nyingine ni ruksa kuchukuliwa kwa kufuata taratibu na pia timu husika kuonana na viongozi wa Simba kumalizana juu ya wachezaji wanaowataka.

``Tumesikia kocha wa watani zetu, Dusan Kondic anamtaka beki wetu Kelvin Yondani kwa gharama yoyote, sisi hatuoni tatizo wala kuwawekea vikwazo ilimradi wafuate taratibu zilizopo,`` Chano alisema.

Alisema kuwa kutakiwa kwa wachezaji wao na watani zao Yanga ni dalili tosha kwamba kikosi chao ni kizuri na chenye wachezaji bora na hivyo ni fahari kwao kwa kuonyesha ni jinsi gani wanazalisha wachezaji wenye ubora unaokubalika.

Kuhusu wao kudaiwa kutaka kuwachukua Jerry Tegete na beki Shadrack Nsajigwa, Chano alisema si kweli kama wana nia ya kuwasajili wachezaji hao kwa madai pamoja na `kupambwa` magazetini kuwa ni mastaa bado hawana kiwango cha kuichezea Simba.

``Hatujui habari hizi zinatoka wapi, lakini ukweli ni kwamba hakuna mchezaji hata mmoja wa Yanga ambaye amefikia kiwango cha kuichezea Simba na tunawatoa hofu watani zetu wala wasisumbuke juu ya hilo kwani hatutamsajili yeyote toka kwao hadi wenye viwango watakapopatikana kwao,`` alisema.

Chano alisema ni kweli wachezaji hao wa Yanga ni wazuri, lakini si kwa kiwango cha kusajiliwa Simba, aliyodai huenda ndio timu yenye kuzalisha na kuwa na wachezaji wenye uwezo wa hali ya juu karibu kila msimu.

Kocha Mkuu wa Yanga Dusn Kondic aliripotiwa na gazeti hili jana akidai kuushinikiza uongozi wa klabu yake kuhakikisha inamsajili Kelvin Yondani pamoja na mchezaji wa Prisons ya Mbeya Stephen Mwasika ikiwa ni moja ya mapendekezo yake ya usajili kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na michuano ya kimataifa.

  • SOURCE: Nipashe
TODAY
-----------------------------------------------
Editorial
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.