|
Mvua yaahirisha mechi Taifa Cup
2008-05-10 10:29:23
By Somoe Ng’itu
Mvua iliyonyesha jana mchana jijini Dar es Salaam imeendelea kusababisha kutochezwa kwa mechi mbalimbali kwenye Uwanja wa Taifa, ambapo jana mechi mbili za mashindano ya Kombe la Taifa ziliahirishwa.
Hali ya mvua ilisababishia hasara Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, ambayo iliileta timu ya taifa ya Msumbiji kuja kucheza mechi ya kirafiki na timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars lakini mechi ilishindwa kuchezwa kutokana na maji kujaa katika uwanja huo wenye nyasi bandia.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa jana mchana saa nane kulitakiwa kuwepo na mechi kati ya mkoa wa Pwani na Kilimanjaro na baadaye kufuatiwa na mchezo kati ya Morogoro na Dodoma.
Taarifa zilizopatikana jijini kutoka kwa mmoja wa viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania zilisema kuwa michezo hiyo sasa inatarajiwa kufanyika leo ambapo mechi ya kwanza itaanza saa mbili na nusu na inayofuata itafanyika saa 4:30 asubuhi.
Akithibitisha kutofanyika kwa michezo hiyo, Meneja wa uwanja huo, Charles Masanja alisema kuwa amewapa taarifa kuwa kutokana na hali iliyojitokeza jana mechi zisingeweza kuchezwa.
Masanja alisema kuwa amejulishwa na Kamati ya Ufundi ya TFF kuwa michezo hiyo itachezwa leo mapema na baadaye kuendelea na ratiba ya mashindano hayo kama ilivyopangwa.
Leo saa nane mchana timu ya mkoa wa Temeke itakutana na mabingwa watetezi wa mashindano hayo, Mbeya huku Mtwara wakiikaribisha Rukwa.
|