|
Simba wamuweka kiporo Henry Joseph
2008-05-10 10:28:34
By Badru Kimwaga
Kamati ya Utendaji ya klabu ya soka ya Simba iliyokuwa ikutane juzi usiku imekwama baada ya baadhi ya viongozi wakuu kushindwa kuhudhuria na hivyo kuweka kiporo hatma ya kiungo wao na nahodha wa timu ya taifa, Henry Joseph aliyesimamishwa kwa tuhuma za utovu wa nidhamu.
Pia kushindwa kufanyika kwa kikao hicho kumefanya hatma ya Mkutano Mkuu unaoliliwa na wanachama kushindwa kufahamika sambamba na suala zima la usajili mpya wa timu na wachezaji wanaotarajiwa kutemwa ndani ya kikosi hicho kilichoshindwa kutetea ubingwa wa Ligi Kuu na hata kukosa nafasi ya kushiriki mashindano ya Afrika msimu ujao.
Mhazini Msaidizi wa klabu hiyo Chano Almasi alisema jana kuwa, kikao cha kamati yao ya utendaji kimeshindwa kufanyika kama kilivyopangwa kutokana na viongozi wakuu wawili kutohudhuria.
Chano aliwataja viongozi walioshindwa kutokea kwenye kikao hicho na kuzuia kufanyika kwake ni Mwenyekiti Hassani Dalali na Makamu wake, Omar Gumbo waliotoa udhuru.
``Tumeshindwa kukutana kama tulivyopanga na mambo yote tuliyokuwa tuyajadili tumeyaweka kiporo hadi wakati mwingine tutakapokutana ikiwemo hatma ya kiungo wetu Henry Joseph na mkutano mkuu,`` Chano alisema.
Henry alisimamishwa na uongozi huo kwa tuhuma za kukacha safari ya timu yao ya Kagera ambako timu hiyo ilikwenda kucheza na Kagera sugar, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, na kikao hicho kingeamua kama asamehewe ama aongezewe adhabu zaidi kulingana na utetezi wake aliotakiwa kuutoa mbele ya kikao hicho.
Chano alisema kuwa, wajumbe waliohudhuria hawakuona vema kuendelea na kikao kama mwenyekiti na makamu wake hawapo na hivyo kukubaliana itafutwe tarehe nyingine ya kuitishwa upya na kujadili masuala hayo pamoja na yale ya usajili mpya wa kikosi chao na tathmini ya ligi kuu iliyomalizika.
Alisema mwenyekiti wao, Hassani Dalali alishindwa kuhudhuria kutokana na kuwa na jukumu la kufuatilia masuala ya usajili na hivyo kushindwa kukiwahi kikao hicho, ingawa hakueleza ni usajili wa wachezaji gani na wa kutoka wapi.
Hatahivyo, mhazini huyo hakuweza kueleza sababu zilizomkwaza makamu wao Omar Gumbo, ila alisema kikao kingine kinatarajiwa kuitishwa haraka hivi karibuni.
|