|
Taifa Cup haiibui vipaji-Minziro
2008-05-10 10:27:49
By Jimmy Charles
Kocha Mkuu wa timu ya mkoa wa Pwani inayoshiriki michuano ya kuwania Kombe la Taifa, Fred Felix Minziro amewaponda wanaodai kuwa michuano hiyo ina lengo la kuibua vipaji.
Minziro, alisema kuwa lengo la michuano hiyo ni kushindana ili mkoa mmoja kati ya 23 kuwa bingwa, ambapo Copa CocaCola ndio michuano maalum ya kuibua vipaji.
Minziro, alitoa kauli hiyo kufuatia baadhi ya wadau wa soka hapa nchini kuzipigia kelele baadhi ya timu zinazoundwa na wachezaji wanaocheza Ligi Kuu.
``Kombe la Taifa toka zamani lengo lake lilikuwa ni kushindana na kuleta umoja baina ya mkoa na mkoa na hatimaye Taifa zima, hii sera ya kuibua vipaji haipo kwenye michuano hii,``alisema Minziro.
Alisema kuwa suala la kutoa nafasi kwa wachezaji chipukizi lifanyike kwenye mashindano ya Copa Coca Cola na si mashindano kama haya ambayo yanazawadi nono kwa mshindi.
Aidha, aliongeza kuwa kuwashirikisha wachezaji wa Ligi Kuu kwenye michuano hiyo kunaleta changamoto na burudani kwa watazamaji kama ilivyokuwa katika mchezo wa juzi kati ya Ilala inayoundwa na nyota wengi wa Simba na Yanga dhidi ya Lindi, ambapo Lindi ilichapwa 10-1.
Minziro ni mmoja wa makocha wa mikoa wanaowatumia wachezaji wengi wa Ligi Kuu kwenye vikosi, ambapo yeye kikosi chake kinaundwa na wachezaji wengi wa JKT Ruvu, ambayo ni timu anayoifundisha.
|