|
Taasisi ya SAEU na uboreshaji Kiingereza
2008-05-06 10:23:26
Na Godfrey Monyo
Suala la matumizi ya lugha za Kiswahili ama Kiingereza katika mitaala ya masomo katika viwango tofauti vya taasisi za elimu nchini, linazidi kujadiliwa kwa namna tofauti, ili kupata suluhu yake. Lakini taasisi ya Southern Africa Extension Unit (SAEU), inayojihusisha, pamoja na mambo mengine, uboreshaji wa sekta ya elimu, inazungumzia na kutekeleza mipango ya uelimishaji wa Kiingereza ili kumudu mawasiliano na ushindani wa kimataifa. Mwandishi Godfrey Monyo, anaandika zaidi katika makala haya.
``Ugumu wa kuelewa na kuzungumza Kiingereza haupo kwa Watanzania tu, bali hata kwa watu wa mataifa mengine, lakini ukweli ni kuwa, hali hiyo inaathiri mfumo wa mawasiliano na ushiriki katika ushindani za soko la kimataifa.``
Hayo ni maneno ya Mkurugenzi wa taasisi ya Southern Africa Extension Unit (SAEU), Bi. Nderikyo Liz Ligate,wakati akielezea umuhimu wa kukielewa Kiingereza.
Kihistoria, Bi. Ligate, alianza kushiriki katika mafunzo ya kiingereza tangu wakati wa harakati za baadhi ya nchi za Kiafrika, ikiwemo Afrika Kusini, kudai uhuru.
Pia, Bi. Ligate amewahi kuandaa na kutekeleza mafunzo ya Kiingereza, Kilimo na Hisabati kwa jamii ya wakimbizi walioingia nchini kutoka kwenye mataifa tofauti.
Anasema Kiingereza kama zilivyo lugha nyingine za kitaifa na kimataifa, hakipaswi kuachwa kwa taasisi za mafunzo pekee, bali ubunifu unaokidhi vigezo vya kitaaluma, unapaswa kufanyika ili kurahisisha mafunzo kwa walengwa.
Hivi sasa, Bi. Ligate kupitia SAEU, ameshiriki kubuni na kuchapisha vitabu maalumu, vinavyoweza kutumika katika madarasa tofauti ya shule za msingi na sekondari, katika kuboresha stadi za kukielewa na kuzungumza kiingereza.
``Vitabu hivi viliwahi kutumika kwa baadhi ya shule za msingi mkoani Kigoma, lakini sasa tumeviboresha na vimekubaliwa na NACTE kutumika kwa wanafunzi,`` anasema.
Ingawa vitabu hivyo havipo katika mitaala ya mafunzo mashuleni, lakini Bi. Ligate anasema kutokana na ruhusa ya NACTE, wanafunzi wanaweza kuvitumia, kwa vile vipo katika mfumo unaokidhi vigezo vya mitaala iliyopo.
Katika majarida ya vitabu hivyo vilivyoanza kusambazwa kwenye baadhi ya shule Jijini Dar es Salaam, kuna nakala kivuli ya waraka wa NACTE, kuruhusu matumizi yake.
Kwa upande mwingine, Bi. Ligate anatoa mfano kuwa, mafunzo kama hayo yaliwahi kuwasaidia sana watoto na watu wazima waliokuwa wakimbizi, ambao waliingia nchini kwa nyakati tofauti, kutokana na vurugu na machafuko nchini kwao.
``Tulikuwa tunahakisha kuwa tunawafundisha kulingana hali halisi…mfano wengi wao walikuwa watu wazima, hivyo tulilazimika kuwatengenezea mtaala uliogusa mambo waliokuwa wakiyafanya kila siku,`` akasema Bi.Ligate.
Wakimbizi hao walikuwa wakifundishwa kiingereza, kilimo na hisabati, kwa kuzingatia uhalisi wa mfumo wa maisha yao.
Sehemu ya wakimbizi hao walikuwa wafungwa wa kisiasa kutoka katika baadhi ya nchi za Afrika kama Afrika Kusini, Zimbabwe na Zambia.
Nchi nyingine walipotoka wakimbizi, waliopata mafunzo hayo ni Rwanda na Burundi, zilizowahi kukabiliwa na machafuko na vita ya wenyewe kwa wenyewe katika kipindi cha muda mrefu.
``Katika machafuko kama hayo, ni wazi kabisa kuwa mambo mengi yalikwenda mrama kiasi cha kufikia hatua, hata mambo ya msingi kama elimu na afya, yalishindwa kupatikana kwa urahisi,`` anasema Bi.Ligate, katika kusisitizia umuhimu wa lugha hiyo.
Anasema vitabu vilivyoandaliwa kwa mafunzo ya kiingereza hapa nchini, vimeandaliwa kwa mfumo usiohitaji ulazima wa kuwapo mwalimu wakati wa kujifunza.
``Mbinu za kitaaluma zilizotumika kuunda vitabu hivi, ni zile zile za utoaji elimu kwa masafa, na ndio maana mbali na vitabu, mafunzo haya yanapatikana kwenye kanda na CD,`` anasema Bi. Ligate, aliyeanzisha taasisi hiyo mwaka 1984, chini ya Sekretarieti ya Nchi za Jumuiya ya Madola (COMSEC).
Kutokana na umuhimu wa mafunzo ya lugha hiyo, ndipo unapoonekana umuhimu wa taasasi kama SAEU, kushiriki katika uboreshaji wa sekta hiyo, iliyo miongoni mwa sekta muhimu katika kufikia maendeleo endelevu.
Anakumbusha kuwa, wakati SAEU inaanza, ilijihusisha zaidi na masuala ya wakimbizi, ikizingatia asili ya uundwaji wake, kupitia COMSEC na kupata msaada kutoka Shirila la Wakimbizi Duniani (UNHCR) na serikali ya Tanzania.
Mkurugenzi huyo akasema, katika kipindi cha miaka ya 1990, taasisi hiyo ilisajiliwa kuwa ya kimataifa, hivyo kujipanua wigo wa uboreshaji na utoaji elimu, na kubuni mahitaji mbalimbali katika sekta hiyo.
``Mwaka 1999 tulifanikiwa kuisajili taasasi yetu na hivyo kuwa ya kimataifa, ambapo tuliweza kufanya kazi kwa mapana zaidi, huku tukibuni mbinu mbadala za kuboresha elimu,``anasema.
Aidha, Bi.Ligate akasema kutokana na jitihada zinazofanywa na serikali katika kuhakikisha kuwa watu wake wanapata elimu, uandaaji, uchapishwaji na usambazaji wa vitabu vilivyoandaliwa na SAEU, ni sehemu ya kuunga mkono jitihada hizo.
``Tumesikia kuwa serikali imeanzisha shule nyingi za kata, lakini shule hizo zina upungufu mkubwa na walimu, vitabu hivi vitakuwa mwongozo na msaada mkubwa kwa wanafunzi,`` akasema.
Kwa mujibu wa Bi. Ligate, mbali na vitabu vya Kiingereza, SAEU imechapisha vitabu vya hisabati kwa wanafunzi wa shule za msingi.
Anasema serikali imewapa idhini ya kufanya majaribio ya vitabu hivyo kwenye shule za msingi Temeke, Madenge , Babati, Ruvuma na Serengeti, wilayani Temeke jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi huyo akasema kuwa vitabu hivyo vinapatikana pia katika mfumo wa sauti na ndio maana vinaweza kutumika bila ya kuwepo kwa mwalimu.
Aliongeza kuwa vitabu hivyo vitaweza kupatikana nchi nzima na sasa na wanajianda kuvizindua ili viweze kuwafikia watu wengi zaid na hasa vijini ambako nipo kuna matatizo makubwa ya walimu pamoja na vitabu vya kusomea jambo ambalo linawafdanya wengi wao kusindwa masomo.
Bi. Ligate akasema anaamini kuwa vitabu hivyo vikitumika ipasavyo, vitaleta mabadiliko kwa wanafunzi, na hivyo kusukuma mbele gurudumu la elimu.
Akasema vitabu kama hivyo, vimewezea kuboresha elimu katika nchi kadhaa, zikiwemo Afrika Kusini , Zimbabwe, Angola na Rwanda.
Hata hivyo, anatoa changamoto kwa serikali, kufanya majaribio na kupima matokeo ya matumizi ya vitabu hivyo.
Anabainisha kuwa, serikali imekuwa ikibadilisha mitaala ya masomo, bila kumaliza kipindi kinachostahili, hivyo kuchangia kurudisha nyuma maendeleo ya elimu nchini.
Kwa upande mwingine anasema serikali imejitahidi kutekeleza shughuli za maendeleo ya elimu, ingawa miongoni mwake zinakwama kutokana na mipango kutokuwa madhubuti ama ushauri mbaya.
``Kila kukicha utakuta serikali imebuni jambo jema, lakini mara nyingi inashindwa kusubiri kuona matunda ya mipango hiyo yanakuwaje, na hasa katika mitaala ya elimu,``anasema.
|