06 May 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Wanafunzi kuanguka: Tunataka maelezo ya kisayansi zaidi
 
2008-05-06 10:22:31
Na Mhariri

Kwa siku kadhaa, wanafunzi wa sekondari na wa shule za msingi wanaripotiwa kuanguka baada ya kupata ugonjwa wa ajabu ambao haujafahamika ukiambatana na kuanguka.

Tatizo la kuanguka kwa wanafunzi limetokea mkoani Dodoma, Shinyanga na pia Kilimanjiro ambayo ni miongoni mwa maeneo machache kati ya mengi yaliyofunga shule na kurudisha wanafunzi majumbani baada ya kuzuka ugonjwa huo `wa ajabu`.

Hata hivyo, sisi tunaona haitoshi kusema wanafunzi wamepata ugonjwa wa kuanguka au wa ajabu ama uliopachikwa jina la kitaalamu mass hysteria (kuchanganyikiwa), na hoja ikaishia hapo.

Tunadhani kwamba maelezo zaidi ya kitalaamu yanahitajika ili kueleza ni kwa nini watoto wanaanguka? Vipimo vya wataalamu vinasemaje?

Kuna nini kwenye viwango vya damu zao? Sukari inatosha mwilini? Au wana malaria, lishe ikoje?

Ni watoto wenye umri gani wanaoanguka au kupata matatizo ya magonjwa ya ajabu na kwa nini wakati huu? Je, kuna misimu maalum ya kuanguka au kupata maradhi hayo?

Hayo ni mambo ambayo wazazi wanataka kusikia ili wajue ni nini hasa kinawasibu watoto na namna ya kuondokana na matatizo kama hayo.

Tunasema hivi kwa sababu nyakati hizi shule nyingi zimefungwa kwa muda kutokana na ugonjwa huo wa ajabu ambao umeripotiwa katika shule za msingi na pia za sekondari, mathalani ya Mnadani mkoani Dodoma ambapo wanafunzi zaidi ya 50 na mwalimu wao walipata ugonjwa huo uitwao `wa ajabu`.

Wakati hayo yakitokea kuna malalamiko ya lishe duni mashuleni. Mathalani wanafunzi wanalalamikia kulishwa chakula kibovu kama ugali wa dona, uji usio na sukari, maharage mabovu na malalamiko mengi kuhusu vyakula. Pengine lishe duni ikawa ndio chanzo cha huo `ugonjwa wa ajabu`.

Tunalazimika kufikiri kuwa pengine hawali vizuri na hawana damu na sukari ya kutosha mwilini au wana matatizo ya minyoo na safura ambayo pia hukausha damu.

Ieleweke kwamba sisi si wataalamu, hiyo tunajaribu tu `kubabia, lakini tunachosema ni kwamba haitoshi kukaa kimya juu ya maradhi hayo bila kuona watalaamu wa afya, wasomi wa ustawi wa jamii na wanasiolojia wakifuatilia na kutueleza ni kipi kinachowatafuna watoto wetu.

Haya madai kuwa shule zimejengwa juu ya makaburi, au kuna majini na maruhani au upo mkono wa mtu si pahali pake katika zama hizi.

Tunasema hivyo kwani yapo pia madai ya shule na vyuo `eti` kufanyiwa mazindiko ili kuepusha matatizo kama hayo na kuchukua.

Huu kwetu ni uduni wa fikra na kuendeleza mambo ya kijima yasiyo kuwa na utaalamu wa kisayansi.

Tunadhani kwamba ni wakati mwafaka kwa Waziri wa Afya na wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuchukua hatua na kutueleza sababu za `maruweruwe` haya mashuleni ambayo yanasababisha mahudhurio duni ya watoto wetu.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.