05 May 2008 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Uzoaji takataka mijini uboreshwe
 
2008-05-05 08:55:16
Na Mhariri

Uamuzi wa kuruhusu shughuli za uzoaji taka katika maeneo mbalimbali mijini Tanzania kufanywa na mawakala bila shaka kulilenga kuziweka shughuli hizi zifanyike kwa ufanisi mzuri zaidi na kuifanya miji hii ipate mandhari za kuvutia.

Na bila shaka ilikuwa ni baada ya kuona halmashauri za miji ama manispaa zikizidiwa na mzigo wa kazi.

Katika misingi hii, kila halmashauri ya wilaya imejikuta ikipata uhuru wa kutangaza na kupata wazabuni wanaokidhi vigezo vinavyostahili katika shughuli hiyo ya usafi wa mazingira.

Ni kwa kuzingatia umuhimu wa mazingira bora kwa maisha ya binadamu, suala hili lilihitaji, na linaendelea kuhitaji mtazamo makini katika uteuzi wa mawakala wa kuifanya kazi hiyo.

Lazima kwanza tukiri kwamba, tunapozungumzia usafi wa mazingira mijini lazima kwanza tuanzie kwa mtu mmoja mmoja jinsi anavyoyathamini mazingira yanayomzunguka.

Wakazi wa miji hii nao wana wajibu mkubwa wa kujifunza au kuendeleza tabia za usafi katika sehemu zote wanazoishi hata kama si nyumbani kwa mhusika.

Mara nyingi inashangaza kuweza kumuona mtu wa makamo, mathalani, akitupa masalio ya matunda katika sehemu yoyote ya wazi hata kama kuna chombo maalumu cha kuweka takataka hizo.

Kumejengeka tabia isiyo njema kwamba hata kama utatupa takataka ovyo, eti wapo watu ambao watakuja kuisafisha, na hivyo kujiondoa kwenye jukumu la kushiriki kuhifadhi mazingira bora.

Sisi tunadhani kwamba kila mkazi ana wajibu wa kubadilika na kuona kwamba njia mojawapo ya kuboresha usafi mijini, ni kwa kila mmoja kuukataa uchafu.

Kwa upande mwingine, halmashauri zinahitajika kuwa makini katika utoaji zabuni kwa makampuni yanayojihusisha na uzoaji taka mijini.

Uzoefu unatuonyesha kwamba, kampuni nyingi za uzoaji taka zina uwezo mdogo mno wa vifaa madhubuti vya uzoaji taka kama vile magari, makasha ya kuhifadhia taka na kadhalika.

Magari ambayo hutumika ni chakavu mno.

Hata watumishi wanaozoa taka hizo nao huwa katika hatari ya kuambukizwa magonjwa kutokana na kukosa vifaa vya kujikinga kiafya.

Ni vizuri halmashauri zikafanya uhakiki wa kutosha kabla ya kumthibitishia mtu aliyeshinda zabuni ya kuzoa taka mahala, tukizingatia kwamba baadhi ya wazabuni hutumia vifaa vya kuazima na visivyo na uhakika.

Halikadhalika, makampuni ya uzoaji taka yalazimike kuwa na uwezo wa kumiliki mapipa imara ya taka ambayo watayakodisha kwa wakazi badala ya mifuko ya plastiki inayotumiwa na watu wengi ambayo hurejesha taka hizo mitaani.

Halmashauri zifuatilie kwa makini kuona kwamba, kampuni ambazo zinashindwa kufuata ratiba au hazina ratiba kabisa za uzoaji taka katika maeneo waliyopangiwa zinafutiwa mikataba mara moja.

Utaratibu wa makampuni hayo kuruhusu baadhi ya maeneo yaliyopo pembezoni mwa barabara kutupiwa takataka kama vituo vya muda unastahili kukomeshwa pia kwani unachangia kuchafua maeneo.

Viongozi wa ngazi za serikali za mitaa nao wanawajibika kuwa makini kuwadhibiti wakazi ambao hutupa takataka kwenye mitaro ya maji na hivyo kusababisha mafuriko nyakati za mvua.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2007 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.