|
Uchaguzi mkuu 2010: CCM ijiandae kwa mjadala wa mageuzi, isitekwe na Ujamaa
2008-05-05 08:54:14
Na Ani Jozeni
Wakati ambapo utawala wa Rais Jakaya Kikwete unakaribia mstari wa kati, au `kipenga` cha `mapumziko` kwa muhula huu wa kwanza, tayari inaelekea chama kimeanza kuwa na sura tofauti na ilivyokuwa katika miaka mingi iliyotangulia.
Wakati ule tofauti za sera au mielekeo ya siasa zilijadiliwa katika vikao vya ndani, wakati chama kilitoa sura moja ya fikra mbele za umma au wafuasi wake kwa jumla.
Suala la kujadili miongoni mwa watu halikuwa ni hizo sera, bali vielelezo tu vya utii kwa chama.
Mpangilio huo wa shughuli za maandalizi ya uchaguzi mkuu inaelekea utabadilika katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu ujao, kwani yale yaliyokuwa yanasemwa miaka iliyopita, kwa mfano na marehemu Horace Kolimba, sasa ndiyo yanaanza kuwa na usahihi wa karibu zaidi.
Hoja ya marehemu Kolimba, katibu mkuu wa zamani wa CCM na Waziri wa Mipango katika kipindi cha pili cha serikali ya awamu ya pili, alitoa rai kuwa CCM imekosa mwelekeo, au sera. Rai hiyo iliwahi kwa takriban miaka kumi.
Chama kukosa mwelekeo siyo kutokuwa na mfumo wa mawazo kifikra au kiitikadi ambao unaridhisha mahitaji ya mtazamo fulani wa maisha, kwa mfano ule wa Ujamaa kwa upande wa hayati Kolimba.
Pia kulikuwa na haja ya kuweka mipaka halisi ya mageuzi ya kiuchumi, na majukumu halisi ya chama kutoa dira kwa wananchi kuhusu dira ya mageuzi ili kuondoa `wasiwasi` wa kuvurugika kwa mfumo mzima wa kile ambacho chama kinatetea.
Hayati Kolimba alikuwa na hoja, ila ziliwahi mno kisiasa.
Kwa hoja kuwa sambamba na mazingira ya kisiasa ni pale chama kinaposhindwa kuhakikisha ule utii wa kawaida, hamasa ya kusikiliza kile wanachosema viongozi wake na kukieleza kwa wananchi wengine.
Kisaikolojia, suala hilo linakuwa na umuhimu kisiasa pale chama kinaposhindwa kuringia kile ambacho chama kinafanya, yaani pale ambapo hata wanachama wenyewe wanaanza kuwa na wasiwasi katika kuringia kile ambacho chama kinafanya.
Kazi ya kukusanya, kuhamasisha, inaanza pia kukwama.
Pamoja na kuwa hali ya kukwama kisera au kisiasa bado haipo katika CCM, nyufa za nini dira inayofaa kufuatwa na nini kinatazamiwa katika utekelezaji wa dira hiyo zinaonyesha kupanuka kwa kiasi kikubwa.
Mjadala wa hivi karibuni wa kufikia au kutekeleza muafaka uliofikiwa na Chama cha Wananchi ilikuwa ni kielelezo, yaani kutoa picha moja kwa wananchi, na halafu kuirudi katika ngazi ya uongozi wa kitaifa. Ina maana hapakuwa na uelekeo halisi wa uongozi katika kufikia muafaka, si wazo tu.
Tatizo lililojitokeza kwa upande wa kufikia na kushindwa kuukubali muafaka limeongezea tu suala la aina gani ya harakati ambazo chama kinatazamiwa kufanya katika uchaguzi mkuu ujao, kwani mpangilio wa 2005 na kwa upande fulani miaka iliyotangulia sasa unasambaratika.
Mgogoro ambao umezuka kuhusu `ufisadi` pale ambako makundi ya biashara yenye washirika katika CCM yameingia ubia na taasisi hii au ile ya kiuchumi imeonekana ni kujitafutia mali.
Wanachama wa CCM au labda hasa ni wa upinzani, wakawarubuni wananchi, wakafuata wabunge, kuzomea biashara.
Matokeo yake ni kuwa chama kimejifunga pingu katika utendaji wake kama serikali, kinaambiwa serikali iache kushirikiana na wafanya biashara kila mahali na badala yake itoe pesa zinazotosha kwa mashirika ya umma kufanya kazi hizo, iwe ni kufua umeme, kuendeleza bandari, au kuchimba mkaa wa mawe.
Ni kana kwamba serikali ilishindwa kuendesha mashirika ya umma lakini inabidi iendelee na sera hiyo, kwani kinyume chake itaanza kushirikiana na wafanyabiashara, jambo ambalo haliwezekani.
Viongozi waandamizi wa awamu hii, na iliyopita, sasa wanasakwa kwa kujihusisha na biashara, ni `mafisadi,` na suala si deni lisilokamilika kulipwa, ila kutaka kupata faida.
Mazingira haya yanafanya mpangilio mzima wa sera ya ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi kuingia katika mashaka makubwa, kwani makubaliano yoyote ambayo yatafikiwa yatakuwa yananufaisha mfanya biashara fulani, na atakuwa ameidhinishwa mkataba huo na ofisa fulani serikalini, na hapo kutakuwa na ufisadi.
Pia ilielezwa nia ya kuondoa kujihusisha na biashara miongoni mwa madiwani, yaani wafanyabiashara wanaokiunga mkono chama wasipewe tenda, ila waratibishe shughuli za wale ambao wanakibeza chama.
CCM haiwezi kuingia katika mchakato wa uchaguzi kwa hali hiyo.
Kinachojitokeza ni kuwa kutakuwa na mparaganyiko wa fikra na uelewa wa kile ambacho chama kinafanya katika kuelekea uchaguzi mkuu, kutokuwepo dira ya pamoja kuhusu mageuzi ya uchumi, kwani upinzani, wahubiri na wasomi wasiotaka kuacha hata chembe ya siasa ya ujamaa wameitia pingu CCM kuwa lazima ifuate siasa isiyochafuliwa na biashara.
Na katika utendaji wa serikali imekuwa vigumu kufikiria kuacha njia za uchumi kushikwa na sekta binafsi, kwani ni rahisi kwa wadadisi wa uelekeo wa Ujamaa, hasa katika Chadema, kugundua kuwa kuna faida kubwa ambayo shirika la umma lingepata kama lingeachiwa lifanye kazi hiyo. Kinyume chake, ufisadi.
Pale ambapo fikra za wananchi pamoja na wabunge wa makundi yaliyoshindana na `mtandao` wa mwaka 2005 wamekubaliana, kwa nia ambayo yenye mchanganyiko wa kutokuelewa matatizo ya kuendesha uchumi kuwa kutumia mashirika ya umma, na pia kutafuta kuungwa mkono na wananchi kuwa wao ni waadilifu na hawatafuti pesa kwa kupitia kushirikiana na wafanyabiashara, uhamasishaji unaweza kuathirika.
Inahitaji kuwa masuala haya ya mageuzi ya uchumi yafafanuliwe ili ule upande unaopendelea mabadiliko uweze kuyatetea miongoni mwa wananchi, ambapo wakati uliopo mfumo wa fikra uliokubaliwa na wasomi na wapinzani ni kufuata siasa ya Ujamaa na kutazamia kuwa ndiyo hapo maendeleo yatapatikana haraka.
Kumbe kinachoharibu maisha ya watu kila siku ni kulundikwa kwa mapesa mengi kwa mahitaji ya mashirika ya umma, Tanesco peke yake ikiwa imechukua shilingi zaidi ya trilioni moja katika bajeti ya mwaka huu.
Ila wasomi hawaoni mizigo hiyo, wanaona viongozi wanaotaka biashara.
Kwa vile malumbano ndani ya Bunge hasa kuhusiana na utendaji serikalini yamekuwa makubwa, na viongozi waandamizi wameaibishwa mbele ya watu kwa dhambi ya kutaka kufanya biashara au kushirikiana na wafanyabiashara, na kwa vile serikali haiwezi kukubali kuwa uchumi uendeshwe kijamaa ili viongozi wasifanye biashara, kuna haja ya kuanzishwa kwa mtandao wa mageuzi katika chama, ili kuhamasisha watu kuendelea na mageuzi yaliyoanza awamu ya pili.
Kuna haja pia ya kupanua wigo la mageuzi hayo kwani yalikwama katika kipindi cha awamu ya tatu, kuzuia fedha kuingia katika nyanja tofauti na kubadili mazingira ya huduma za msingi za biashara (reli, umeme, posta na simu, n.k.) na sasa wasomi wanataka kung’oa hata kile kidogo ambacho kilifanyika, badala ya kuendeleza mageuzi na kuweka miundombinu inayoendana na nchi zinazoendelea kwa kasi.
Ni mpangilio wa sera unaoiumiza CCM.
|